Maelfu ya wakimbizi mashariki mwa Congo DR wanahitajia misaada ya kibinadamu
Maelfu ya wakimbizi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanahitajia misaada ya kibinadamu.
Hubert Kanza Vumba kiongozi wa eneo la Kabalo katika mkoa wa Tanganyika ulioko mashariki mwa nchi hiyo amesema kuwa, wakimbizi takribani elfu nne wa eneo hilo wanakabiliwa na hali mbaya ya kimaisha na kwamba, wanahitajia misaada ya kibvinadamu.
Hubert Kanza Vumba amesema kuwa, raia hao wameyakimbia makazi yao baada ya kuzuka mapigano kati ya wanamgambo wa Luba na Pygmy. Afisa huyo wa serikali ameongeza kuwa, harakati za wanamgambo hao zimefanya suala la upelekaji misaada kwa raia hao kuwa gumu.
Dieudonne Yumba mmoja wa maafisa wa serikali katika mkoa wa Tanganyika ametangaza kuwa, kundi la kwanza la kikosi cha jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo limewasili katika eneo la Kongolo katika mkoa wa Katanga likiwa tayari kwa ajili ya kurejesha amani na usalama katika maeneo yaliyokumbwa na ukosefu wa usalama.
Mapigano ya kikabila yamekuwa yakijiri mara kwa mara katika eneo hilo la Kabalo mkoani Tanganyika na kusababisha mauaji ya watu.
Eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo limekuwa likishuhudia machafuko kwa zaidi ya miaka 20 sasa kutokana na kuwa ngome ya makundi kadhaa ya waasi kutoka nchi jirani za Rwanda na Uganda.
Ukosefu wa usalama katika maeneo hayo umepelekea raia wengi walazimike kuyakimbia makazi yao.