Mripuko wa Bomu wautikisa mji wa Mogadishu
Mtu moja ameuawa na wengine wawili wamejeruhiwa katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu wakati bomu lilipolipuka jana Jumapili, karibu na kambi ya wakimbizi.
Afisa wa ngazi za juu katika idara ya polisi Ibrahim Elmi amesema, mlipuko huo umejiri katika wilaya ya Bondeere, karibu na kambi ya mamia ya wakimbizi wa ndani ya nchi.
Hakuna kundi lolote lililodai kuhusika na hujuma hiyo lakini magaidi wa ash Shabab hufanya mashambulizi kama hayo mara kwa mara nchini Somalia.

Hayo yanajiri wakati ambapo magaidi wa ash Shabab wenye uhusiano na mtandao wa kigaidi wa al Qaida wamedai kuudhibiti mji mmoja wa kiistratejia katikati mwa Somalia baada ya mamia ya wanajeshi wa Ethiopia wanaohudumu katika kikosi cha kulinda amani cha umoja wa Afrika huko Somalia (AMISOM) kuondoka katika mji huo.
Hii ni mara ya tatu mwezi huu ambapo wanamgambo wa ash Shabab wameingia katika mji huo baada ya wanajeshi wa Ethiopia kuondoka katika mji huo. Taarifa ya kundi la ash Shabab imeeleza kuwa wapiganaji wa kundi hilo wameudhibiti kikamilifu mji wa Halgan baada ya askari wa Amisom ambao wametajwa kuwa maadui kuondoka katika mji huo.