Wakongomani walio wengi hawataki Katiba ibadilishwe kwa maslahi ya Rais Kabila
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i18145-wakongomani_walio_wengi_hawataki_katiba_ibadilishwe_kwa_maslahi_ya_rais_kabila
Matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yanaonyesha kuwa raia wengi wanapinga Katiba ya nchi hiyo kufanyiwa mabadiliko.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Oct 25, 2016 13:09 UTC
  • Wakongomani walio wengi hawataki Katiba ibadilishwe kwa maslahi ya Rais Kabila

Matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yanaonyesha kuwa raia wengi wanapinga Katiba ya nchi hiyo kufanyiwa mabadiliko.

Matokeo ya uchunguzi huo wa maoni uliofanywa na Chuo Kikuu cha New York cha Marekani kwa ushirikiano na Taasisi ya Uchunguzi wa Maoni ya Kongo yanaonyesha kuwa akthari ya Wakongomani wanapinga Katiba kufanyiwa mabadiliko kwa manufaa ya Rais wa nchi hiyo Joseph Kabila ili kumwezesha aendelee kubakia madarakani kwa muhula wa tatu na wanaitakidi kuwa kiongozi huyo anapaswa kung'atuka madarakani ifikapo mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka huu.

Zaidi ya asilimia 81 ya watu waliotoa maoni yao wamepinga Katiba kufanyiwa mabadiliko na Rais Kabila kuendelea kubakia madarakani; na asilimia 74 ya Wakongomani wamesema kiongozi huyo inapasa aondoke madarakani mwishoni mwa mwaka huu.

Uchunguzi huo wa maoni aidha umeonyesha kuwa umashuhuri wa Kabila, ambaye katika uchaguzi wa mwaka 2011 alishinda kwa kujipatia asilimia 48.9 ya kura umepungua kwa kiwango kikubwa.

Ghasia za maandamano ya Kinshasa

Zoezi hilo la uchunguzi wa maoni lilifanyika katika kipindi cha kati ya mwezi Mei na Septemba katika mikoa 26 ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kushirikisha watu 7,545.

Tangu ijipatie uhuru wake mwaka 1960, Kongo DR iliyowahi pia kujulikana kwa jina la Zaire haijawahi kushuhudia mabadiliko ya uongozi wa juu wa kisiasa kwa njia za amani.

Inafaa kukumbusha hapa kuwa makumi ya watu waliuawa katika maandamano ya mwezi uliopita katika mji mkuu Kinshasa ya kupinga kuahirishwa uchaguzi wa rais na kumwezesha Rais Kabila kuendelea kubaki madarakani.../