Gambia nayo yatangaza azma yake ya kujiondoa ICC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i18196-gambia_nayo_yatangaza_azma_yake_ya_kujiondoa_icc
Gambia imejiunga na nchi kadhaa za Afrika zilizotangaza azma yao ya kujiondoa katika Mkataba wa Roma uliobuni Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 26, 2016 11:26 UTC
  • Gambia nayo yatangaza azma yake ya kujiondoa ICC

Gambia imejiunga na nchi kadhaa za Afrika zilizotangaza azma yao ya kujiondoa katika Mkataba wa Roma uliobuni Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC.

Sheriff Bojang, Waziri wa Habari wa Gambia amesema nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika inaazimia kujiondoa ICC kutokana na kile alichokitaja kuwa, mahakama hiyo iliyoko mjini Hague nchini Uholanzi inatumika kuwahujumu na kuwadhalilisha viongozi wa Afrika.

Rais wa Gambia Yahya Jameh

Akitoa mfano wa namna mahakama hiyo inavyofumbia macho jinai zinazofanywa na viongozi wa nchi za Magharibi, Waziri wa Habari wa Gambia amesema iwapo mahakama hiyo ingelikuwa na uadilifu, ingelikuwa imemfungulia mashtaka Tony Blair, Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, kutokana na jinai za kivita nchini Iraq mwaka 2003.

Haya yanajiri siku chache baada ya Rais Yoweri Museveni wa Uganda kupongeza uamuzi wa Afrika Kusini kuanzisha mchakato wa kujiondoa ICC na kusema kuwa, uamuzi huo ni 'mzuri mno' na kwamba "ICC haina maana." Hata hivyo Rais Museveni alikwepa swali la wanahabari walipomuuliza iwapo Uganda itafuata mkondo huo wa Afrika Kusini na Burundi wa kujiondoa katika Mkataba wa Roma uliobuni mahakama hiyo iliyoko mjini Hague nchini Uholanzi.

Nkosazana Dlamini-Zuma, Mkuu wa Kamisheni ya AU

Hii ni katika hali ambayo, Nkosazana Dlamini Zuma, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amesema, umoja huo haujatangaza msimamo wowote kuhusiana na wimbi hilo la nchi za Afrika kujiondoa ICC na kusisitiza kuwa, uamuzi huo unafaa kuchukuliwa na nchi husika.

Nchi kadhaa za Kiafrika zimetishia kujiondoa kwenye mahakama hiyo kutokana na hatua yake ya kuendelea kuwasakama viongozi wa nchi za bara hilo, huku ikifumbia macho jinai zinazofanywa na viongozi wa Magharibi.