Wanaharakati kadhaa wa kijamii wakamatwa DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i18208-wanaharakati_kadhaa_wa_kijamii_wakamatwa_drc
Wanaharakati kadhaa wa masuala ya kijamii wametiwa mbaroni huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya kutuma barua kwa askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kulalamikia makubaliano ya kisiasa yaliyofikiwa hivi karibuni kati ya serikali na baadhi ya wapinzani nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 26, 2016 11:49 UTC
  • Wanaharakati kadhaa wa kijamii wakamatwa DRC

Wanaharakati kadhaa wa masuala ya kijamii wametiwa mbaroni huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya kutuma barua kwa askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kulalamikia makubaliano ya kisiasa yaliyofikiwa hivi karibuni kati ya serikali na baadhi ya wapinzani nchini humo.

Maafisa wa polisi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo leo Jumatano wamewatia mbaroni wanaharakati wanane wa asasi ya kijamii ya Lucha wakiwa mbele ya kituo cha askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa huko Goma, makao makuu ya mkoa wa Kivu Kaskazini, mashariki mwa DRC.

Wanaharakati hao wanalalamikia makubaliano yaliyofikiwa tarehe 18 mwezi huu wa Oktoba baina ya Rais Joseph Kabila na vyama na makundi ya upinzani kuhusu kurefushwa muda wa urais wake ili kutoa mwanya wa kufanyika uchaguzi mkuu mwezi Aprili 2018 kwa ufanisi zaidi.

Maandamano ya wapinzani mjini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

 

Muda wa urais wa Joseph Kabila unamalizika tarehe 20 Disemba mwaka huu na wanaharakati hao wanamtaka Kabila aondoke madarakani mara muda wake utakapomalizika. 

Wanaharakati 9 wengine wa harakati hiyo walitiwa mbaroni juzi Jumatatu na jana Jumanne mjini Goma. Harakati hiyo imelaani hatua ya kutiwa mbaroni wanachama wake hao. Hata hivyo Vital Umiya Awashango, afisa mwanadamizi wa polisi katika mkoa wa Kivu Kaskazini amesema kuwa, watu hao wametiwa mbaroni kwa kujaribu kuvuruga usalama wa nchi hiyo.