Waasi wa Maï-Maï watakiwa kuweka chini silaha DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i18304-waasi_wa_maï_maï_watakiwa_kuweka_chini_silaha_drc
Jumuiya za kiraia katika mkoa wa Kivu Kaskazini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, zimewataka waasi wa Maï-Maï kuweka chini silaha zao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 28, 2016 03:53 UTC
  • Waasi wa  Maï-Maï watakiwa kuweka chini silaha DRC

Jumuiya za kiraia katika mkoa wa Kivu Kaskazini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, zimewataka waasi wa Maï-Maï kuweka chini silaha zao.

Jumuiya hizo za kiraia zimelitaka jeshi la nchi hiyo kwa kushirikiana na askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Mataifa kuendesha operesheni kubwa kwa lengo la kuwanyang'anya silaha waasi hao wanaoendesha harakati zao katika maeneo ya Rutshuru na Lubero kwenye mkoa wa Kivu Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kadhalika jumuiya hizo zimeonyesha wasi wasi wake juu ya kuzuka mgogoro baina ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Uganda, kufuatia mashambulizi ya waasi hao wa Maï-Maï.

Askari wa serikali ya Kongo DR wakijaribu kukabiliana na waasi

Mbali na hayo, jumuiya hizo za kiraia zimewatuhumu viongozi wa waasi hao kwa kupora mali za raia wa nchi hiyo. Ndjike Kaiko, msemaji wa moja ya jumuiya hizo amenukuliwa akielezea, kuwepo mipango ya kuanzishwa operesheni kabambe dhidi ya waasi hao. Itafaa kuashiria kuwa, maeneo ya mashariki na kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yamekuwa yakishuhudia machafuko kwa kipindi cha miaka 20 sasa, huku udhaifu wa jeshi la serikali na askari wa kofia ya buluu wa Umoja wa Mataifa, vikitajwa kuwa sababu kuu ya kadhia hiyo.