Wakfu wa Mandela wamsuta Zuma, wasema ameshindwa na uongozi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i18607-wakfu_wa_mandela_wamsuta_zuma_wasema_ameshindwa_na_uongozi
Wakfu wa Mandela umemjia juu Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma anayekabiliwa na mashinikizo yanayomtaka ajiuzulu kutokana na tuhuma za ufisadi zinazomundama na utumiaji mbaya wa mamlaka yake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 01, 2016 11:14 UTC
  • Wakfu wa Mandela wamsuta Zuma, wasema ameshindwa na uongozi

Wakfu wa Mandela umemjia juu Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma anayekabiliwa na mashinikizo yanayomtaka ajiuzulu kutokana na tuhuma za ufisadi zinazomundama na utumiaji mbaya wa mamlaka yake.

Wakfu wa Mandela ambao uliazishwa kwa ajili ya kulinda turathi, historia na mafanikio ya hayati Nelson Mandela, rais wa zamani wa nchi hiyo, umesema serikali ya Zuma imeshindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kwamba 'magurudumu ya taifa hilo yanaelekea kung'oka'.

Hayati Nelson Mandela, rais wa zamani wa Afrika Kusini

Taarifa ya wakfu huo imekitaka chama tawala ANC kuchukua hatua za dharura na za makusudi ili kulirejesha taifa hilo la kusini mwa Afrika katika nafasi na haiba yake kieneo na kimataifa. Kwa njia isiyo ya moja kwa moja, Wakfu wa Mandela umetaka kufanyika mageuzi ndani ya uongozi wa chama hicho.

Wito wa taasisi hiyo umeungwa mkono na Ndileka Mandela, mjukuu wa mzee Mandela, katika hatua ambayo inaonekana kuwa pigo kwa Rais Zuma na chama cha ANC.

Maandamano dhidi ya Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini

Hivi karibuni wafuasi wa chama tawala cha ANC waliandamana mbele ya makao makuu ya chama hicho huko Johannesburg wakitaka kujiuzulu Zuma, baada ya kufanya vibaya katika uchaguzi wa mabaraza ya miji, sambamba na kuandamwa na kesi zaidi ya 700 za ufisadi wa kifedha.

Mwezi Machi mwaka huu, Mahakama ya Katiba ya Afrika Kusini ilimuamuru Zuma arejeshe dola milioni 16 fedha za umma alizotumia kukarabati nyumba yake ya kifahari katika eneo la KwaZulu Natal; hatua iliyozusha makelele na malalamiko ya kumtaka ajiuzulu.