Hali yazidi kuwa tete Benin, maandamano yamechachamaa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i18865-hali_yazidi_kuwa_tete_benin_maandamano_yamechachamaa
Maandamano ya kumuunga mkono mgombea wa zamani wa urais wa Benin yamechachamaa katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 05, 2016 11:33 UTC
  • Hali yazidi kuwa tete Benin, maandamano yamechachamaa

Maandamano ya kumuunga mkono mgombea wa zamani wa urais wa Benin yamechachamaa katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Shirika la habari la Africanews limeripoti habari hiyo leo na kuongeza kuwa, hayo ni maandamano ya wafuasi wa Sebastien Ajavon, mfanyabiashara maarufu na ambaye aliwahi kuwa mgombea wa urais wa nchi hiyo. Maandamano hayo yamefanyika sambamba na tangazo la mahakama ya Benin la kumtoa hatiani mfanyabiashara huyo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mahakama ya Benini imemtoa hatiani Sebastien Ajavon na wenzake watatu waliokuwa wametiwa mbaroni jana Ijumaa kwa tuhuma za kufanya magendo ya mihadarati.

Taarifa kutoka Benin zinasema kuwa, waandamanaji walikuwa wamebeba maberamu yaliyoonesha kufurashishwa kwao na kutolewa hatiani kiongozi wao huyo na vile vile kulaani duru zilizowahusisha na magendo hayo. 

Sebastien Ajavon, mfanyabiashara maarufu na ambaye aliwahi kuwa mgombea wa urais wa Benin

 

Benin imekuwa katika mgogoro wa kiuchumi kwa muda mrefu, hususan baada ya nchi jirani zake kama vile Nigeria kukumbwa na mgogoro wa kiuchumi uliotokana na kuporomoka vibaya bei ya mafuta katika soko la dunia. 

Benin ilipata uhuru wake mwaka 1960 kutoka kwa mkoloni mkongwe wa Ulaya, yaani Ufaransa. Ushindani wa kisiasa umechachamaa hivi sasa nchini humo, kiasi kwamba mgombea huyo wa zamani wa urais amewashambulia vikali wapinzani wake kuwa wanafanya njama za kummaliza kisiasa kwa tuhuma zisizo na msingi kama hizo za kufanya magendo ya mihadarati.