Malalamiko ya wananchi yaongezeka nchini Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i18922-malalamiko_ya_wananchi_yaongezeka_nchini_sudan
Malalamiko ya wananchi yameongezeka mjini Khartoum Sudan baada ya serikali ya nchi hiyo kupandisha bei ya nishati.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 06, 2016 09:56 UTC
  • Rais Omar al Bashir wa Sudan
    Rais Omar al Bashir wa Sudan

Malalamiko ya wananchi yameongezeka mjini Khartoum Sudan baada ya serikali ya nchi hiyo kupandisha bei ya nishati.

Shirika la habari la IRNA limeripoti leo kuwa, malalamiko ya wakazi wa mji wa Khartoum dhidi ya hatua ya serikali ya Sudan ya kupandisha bei ya mafuta na umeme yanazidi kuongezeka huku polisi wa nchi hiyo wakimtia mbaroni Khalid Omar Yusuf, mmoja wa viongozi waandamizi wa mrengo wa upinzani.

Wapinzani nchini Sudan wametoa tamko leo Jumapili na kusema kuwa wataendelea na upinzani wao dhidi ya serikali hata kama kiongozi wao mwanadamizi ametiwa mbaroni na vyombo vya dola.

Khartoum, mji mkuu wa Sudan

 

Wapinzani hao wameongeza kuwa, siasa za marekebisho ya kiuchumi za serikali ya Rais Omar al Bashir hazikubaliki na inabidi wananchi wa Sudan wasimame kidete kuzipinga. Wapinzani hao wametoa mwito wa mgomo wa taifa kulalamikia kupandishwa bei ya nishati nchini Sudan.

Hivi sasa polisi na taasisi nyingine za usalama zimewekwa katika hali ya tahadhari ili kuzuia kuzuka wimbi jipya la malalamiko ya wananchi nchini Sudan.

Kabla ya hapo, madaktari walifanya mgomo nchini Sudan kulalamikia kutotimiziwa matakwa yao.

Takwimu za taasisi za kimataifa zinaonesha kuwa, hivi sasa Sudan iko katika hali ya hatari sana katika upande wa njaa na uchache wa chakula.