Al Shabab wadai kuripua bomu karibu na bunge la Somalia
Kundi la kigaidi la al Shabab limedai kuhusika na hujuma ya bomu la kutegwa garini karibu na bunge la Somalia mjini Mogadishu ambapo wanajeshi wawili wa Kisomali waliuawa na wengine watano kujeruhiwa.
Magaidi wa al Shabab wamezidisha hujuma zao za mabomu mjini Mogadishu huku uchaguzi wa bunge ukikaribia nchini humo.
Msemaji wa kundi hilo Sheikh Abdiasis Abu Musab amedai kuwa wanajeshi 17 waliuawa katika hujuma hiyo lakini afisa wa ngazi za juu wa Polisi ya Somalia Kanali Abdiqadir Hussein amesema ni wanajeshi wawili waliouawa.
Hujuma hiyo imekuja siku moja baada ya Umoja wa Mataifa kuonya kuwa, magaidi wakufurishaji wa kundi la al Shabab ni tishio kubwa sana kwa nchi ya Somalia na eneo zima la mashariki mwa Afrika.

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa imeonya kuwa, magaidi wa al Shabab walioko Somalia bado wana uwezo wa kufanya mashambulizi makubwa pamoja na kuwepo taarifa za mafanikio katika jitihada za kupambana na ugaidi nchini humo.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa al Shabab ni hatari kwa usalama na utulivu Somalia na pia linaendelea kuvuruga usalama katika eneo zima la Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika.