Kampala yatangazwa kuwa mji bora zaidi Afrika Mashariki
Utafiti uliofanywa na taasisi ya Mercer unaonyesha kuwa, jiji la Kampala nchini Uganda ndilo bora zaidi kwa ajili ya kuishi katika eneo la Afrika Mashariki.
Utafiti huo unaonyesha kuwa, ughali wa maisha ni wa kiwango cha wastani na usalama pia ni wa kuridhisha katika jiji la Kampala.
Ingawa Kampala umetajwa kuwa mji bora wa kuishi Afrika Mashariki, lakini haujaweza kupata nafasi ya kuingia kwenye miji 100 bora duniani. Cape Town na Johannesburg ya Afrika Kusini ndiyo miji ya pekee kutoka Afrika ambayo imefanikiwa kuingia kwenye orodha ya 100 bora. Cape Town inashikilia nafasi ya 92 nayo Johannesburg inashikilia nafasi ya 95 duniani.
Mji mkuu wa Austria, Vienna umetajwa kuwa mji bora zaidi kuishi duniani. Miji mingi kwenye orodha ya 100 bora ni kutoka Ulaya, Amerika na Asia Mashariki. Mji mkuu wa Iraq, Baghdad ndio uanoburuza mkia kwenye utafiti huo na umetajwa kuwa mji mbaya na hatari zaidi kuishi duniani.