Makumi ya wanachama wa Boko Haram wauawa Cameroon
Jeshi la Cameroon limewaangamiza makumi ya wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo.
Vyombo vya usalama vya Cameroon vimetangaza kuwa, jeshi la nchi hiyo limefanikiwa kuwaangamiza wanachama wasiopungua 20 wa kundi la Boko Haram katika operesheni iliyofanyika kwenye eneo la Sandawadjirin huko kaskazini mwa nchi hiyo. Wanachama wengine wengi wa kundi hilo wamejeruhiwa.
Wanachama wa kundi hilo wameuawa wakati walipokuwa wakijitayarisha kufanya mashambulizi dhidi ya kambi moja ya jeshi la Cameroon. Katika siku za hivi karibuni kundi la Boko Haram limeelekeza zaidi mashambulizi yake ya kigaidi katika kambi za jeshi la Cameroon.
Kundi la wakufurishaji la Boko Haram lilianzisha mashambulizi kaskazini mwa Nigeria miaka saba iliyopita na hadi hivi sasa watu wasiopungua 20 elfu wameshauawa na zaidi ya milioni mbili na laki sita wengine wameshapoteza makazi yao. Katika miaka ya hivi karibuni kundi hilo limepanua zaidi mashambulizi yake katika nchi jirani kama Cameroon, Chad na Niger