Umoja wa Mataifa wataka kuheshimiwa haki za waandamanaji Congo DR
Umoja wa Mataifa umeitaka serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuheshimu haki za kimsingi za raia wa nchi hiyo.
Takwa hilo limetolewa na ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa uliotumwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika mazungumzo yake na Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo. Ujumbe huo wa Baraza la Usalama umemtaka Rais Joseph Kabila kukaa katika meza ya mazungumzo na wapinzani na wakati huo huo, serikali yake iheshimu haki za raia ikiwemo haki ya kufanya maandamano.
Ujumbe huo umesema kuwa, kuendelea mwenendo wa sasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wa kupigwa marufuku upinzani kwa njia za amani ni jambo linalotia wasiwasi.
Ujumbe wa wawakilishi 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa uliowasili Kinshasa Ijumaa ya juzi utaendelea kuwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hadi kesho Jumatatu.
Mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hivi karibuni uliingia katika hatua mpya baada ya Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo kutangaza kuwa, uchaguzi wa Rais nchini humo utafanyika mwaka 2018 kutokana na kile kilichoelezwa kuwa kutokamilika kwa maandalizi ya kutosha kwa ajili ya kuendesha zoezi la uchaguzi huo.
Ikumbukwe kuwa, makumi ya watu waliuawa katika maandamano ya mwezi Septemba mwaka huu katika mji mkuu Kinshasa ya kupinga kuahirishwa uchaguzi wa rais na kumwezesha Rais Kabila kuendelea kubaki madarakani.