Uholanzi yawarejesha Rwanda washukiwa 2 wa mauaji ya kimbari
Uholanzi imewarejesha nchini mwao washukiwa wawili wa mauaji ya kimbari yaliyotokea nchini Rwanda mwaka 1994.
Jean-Claude Iyamuremye na Jean-Baptiste Mugimba wamerejeshwa nchini Rwanda kufuatia uamuzi uliotolewa na mahakama moja nchini Uholanzi. Wawili hao wanatuhumiwa kuhusika na mauaji hayo ya kimbari dhidi ya Watutsi mwaka 1994 ambapo pamoja na mashtaka mengine, wanakabiliwa na shitaka la jinai dhidi ya binadamu.
Kamisheni ya Taifa ya Kupambana na Mauaji ya Kimbari nchini Rwanda imeipongeza serikali ya Uholanzi kwa kuunga mkono mchakato wa haki na wa kuwarejesha washukiwa hao nchini.
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Rwanda, Richard Muhumuza, amethibitisha habari hizo na kusema kuwa washukiwa hao kwa sasa wanazuiliwa katika gereza kuu la Kigali na kwamba karibuni hivi watapandishwa kizimbani.
Mwezi Machi mwaka huu, Ladislas Ntaganzwa ambaye anayetuhumiwa kuhusika na mauaji ya kimbari yaliyofanyika mwaka 1994 nchini Rwanda alikabidhiwa kwa vyombo vya mahakama ya nchi hiyo baada ya kukamatwa nchini Kongo DR mwaka jana. Ladislas Ntaganzwa ambaye alitiwa nguvuni nchini Kongo Disemba 9 mwaka jana alikuwa meya wa zamani wa eneo la Nyakizu ambako inasemekana alifanya mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi.
Kwa akali Watutsi na Wahutu wenye misimamo ya wastani wapatao laki nane waliuawa kinyama mwaka 1994 katika kipindi cha siku 100 nchini Rwanda, jinai ambazo zilifanywa na Wahutu wenye misimamo mikali mbele ya askari wa kofia buluu wa Umoja wa Mataifa.