Watu 15 wauawa katika mapigano mapya Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i19696-watu_15_wauawa_katika_mapigano_mapya_sudan_kusini
Kwa akali watu 15 wameuawa katika makabiliano mapya kati ya jeshi la serikali na waasi, katika kijiji cha Adaab el Bahr, Jimbo la Unity, nchini Sudan Kusini karibu na mpaka wa pamoja na Sudan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 18, 2016 04:08 UTC
  • Watu 15 wauawa katika mapigano mapya Sudan Kusini

Kwa akali watu 15 wameuawa katika makabiliano mapya kati ya jeshi la serikali na waasi, katika kijiji cha Adaab el Bahr, Jimbo la Unity, nchini Sudan Kusini karibu na mpaka wa pamoja na Sudan.

Kanali Santo Dominic Chol, naibu msemaji wa jeshi la nchi hiyo amesema mapigano yalianza baada ya wapiganaji wa Makamu wa Rais wa zamani Riek Machar kuvamia kijiji hicho na kujirabu kuiba mifugo kabla ya kushambuliwa na askari wa serikali.

Hata hivyo, Meja Dickson Gatluak Jock, msemaji wa waasi wanaomuunga mkono Machar amesema wapiganaji wa SPLA wameuawa askari 20 wa serikali katika kijiji cha Adaab el Bahr, na wengine 23 katika eneo la Tore.

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir na aliyekuwa Makamu wake Riek Machar

Haya yanajiri masaa machache baada ya Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kutahadharisha kuhusu uwezekano wa kufanyika jinai kubwa nchini Sudan Kusini.

Aidha wiki iliyopita, Adama Dieng, mshauri maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya kuzuia mauaji ya kimbari alisema kuwa, wimbi la mauaji ya kikabila linaloshuhudiwa nchini Sudan Kusini kwa sasa linatia wasiwasi na kubainisha kuwa, uchunguzi wao umebaini kuwa mauaji ya kikabila yanayoshuhudiwa ni dhihirisho kuwa mchakato wa kushuhudiwa mauaji ya kimbari nchini humo unatokota.