Lori la mafuta laripuka na kuua watu 73 nchini Msumbiji
Zaidi ya watu 70 wamepoteza maisha baada ya lori la mafuta kuripuka katika mji wa Caphiridzange, mkoa wa Tete kaskazini mwa Msumbiji.
Habari zinasema kuwa, watu 73 wameaga dunia na wengine 110 kupata majeraha mabaya ya kuungua, baada ya lori hilo la mafuta kuripuka na kushika moto.
Habari zaidi zinasema kuwa, akthari ya waliopoteza maisha katika mkasa huo wa jana jioni ni watu waliokuwa wamelizingira lori hilo wakinunua mafuta kutoka kwa dereva wake.
Serikali ya Msumbiji imetuma timu ya maafisa wake kwenda kwenye eneo la tukio kutathmini hali huku ikiarifiwa kuwa, yumkini idadi ya walioaga dunia ikaongezeka kutokana na majeraha mabaya waliyoyapata manusura wa ajali hiyo.
Vyombo vya dola vimeanzisha uchunguzi kubaini kiini cha mripuko huo, lakini baadhi ya mashuhuda wanasema moto huo ulianza baada ya radi na umeme kulipiga lori hilo la mafuta lililokuwa likitoka katika nchi jirani ya Malawi, wakati watu walikuwa wanachota mafuta.
Wengine wanasema kuwa, moto mdogo uliokuwa ukiwaka pembeni mwa lori hilo, ndio uliosababisha mripuko huo baada ya watu kuanza kuchota mafuta.
Baadhi ya manusuru wanaripotiwa kujirusha katika mto mmoja ulioko karibu na eneo palipotokea ajali hiyo ili kuyanusuru maisha yao.