Jumuiya za misaada ya kibinadamu: Somalia inakabiliwa na njaa
Mamilioni ya raia wa Somalia wanakabiliwa na hatari ya ukosefu wa chakula na baa la njaa.
Hayo yametangazwa na jumuia 38 za misaada ya kibinadamu katika taarifa ya pamoja uliyotolewa mjini Mogadishu. Taarifa hiyo imesema: Kwa kutilia maanani uhaba wa mvua, ukame na ukosefu wa chakula, Wasomali wasiopungua milioni tano wanakabiliwa na hatari ya baa la njaa.
Jumuiya hizo zimetangaza kuwa, hali hiyo imeathiri vibaya mazao ya chakula na maji ya kunywa nchini Somalia.
Ripoti ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) inasema kuwa, zaidi ya watu milioni moja na laki moja wa Somalia hawana uwezo wa kukidhi mahitaji yao ya chakula na wengine milioni 3 na laki 9 wanapata mashaka makubwa kukidhi mahitaji hayo.
Eneo la Pembe ya Afrika linasumbuliwa na ukame ambao unasababisha vifo vya wanyama na uharibifu wa mazao ya kilimo.