Tahadhari ya UN kuhusu vifo vya watoto Nigeria
Umoja wa Mataifa umetahadahrisha kuwa, hujuma za kigaidi za Boko Haram ni chanzo cha familia kuwa wakimbizi Nigeria na hivyo kusababisha vifo vya makumi ya maelefu ya watoto nchini humo.
Katika taarifa, Umoja wa Mataifa umesema makumi ya maelefu ya watoto kaskazini mashariki mwa Nigeria wanakabiliwa na hatari ya kifo kila siku kutokana na vita, njaa na lishe duni.
Ripoti hiyo imesema kuwa maeneo yanayodhibitiwa na Boko Haram yana idadi ya watu milioni 14 wanaohitajia msaada wa kibinadamu na kwamba kuna hatari ya watoto 17 elfu kupoteza maisha eneo hilo mwaka 2017.
Tokea Boko Haram ianzishe uasi wake Nigeria mwaka 2009, watu elfu 20 wamepoteza maisha. Aidha zaidi ya watu milioni mbili wamefanywa wakimbizi kufuatia ugaidi wa Boko Haram.
Neno Boko Haram kwa lugha ya Kihausa lina maana ya 'elimu kutoka nchi za Magharibi ni haramu'. Kundi hilo la Boko Haram ambalo lina ufahamu usio sahihi na potovu kuhusu dini ya Kiislamu, limekuwa likitekeleza hujuma katika maeneo mbalimbali ya Nigeria hasa kaskazini mwa nchi hiyo.