Mahakama ya Kijeshi Rwanda yaanza kusikiliza kesi ya Seyoboka
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i20554-mahakama_ya_kijeshi_rwanda_yaanza_kusikiliza_kesi_ya_seyoboka
Mahakama ya Kijeshi ya Rwanda leo imeanza kusikiliza kesi ya afisa wa zamani wa jeshi la nchi hiyo aliyerejeshwa nyumbani kutoka Canada mwezi uliopita kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya kimbari ya 1994.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 01, 2016 11:30 UTC
  • Mahakama ya Kijeshi Rwanda yaanza kusikiliza kesi ya Seyoboka

Mahakama ya Kijeshi ya Rwanda leo imeanza kusikiliza kesi ya afisa wa zamani wa jeshi la nchi hiyo aliyerejeshwa nyumbani kutoka Canada mwezi uliopita kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya kimbari ya 1994.

Jean Claude Seyoboka anatuhumiwa kufanya mauaji ya kimbari, kupanga mauaji hayo, ubakaji na kutenda jinai nyingine dhidi ya binadamu.

Seyoboka ambaye alikuwa Luteni wa Pili wa jeshi wakati kundi lisilojulikana hadi sasa lilipoangusha ndege iliyokuwa imembeba rais wa zamani wa Rwanda Juvenal Habyarimana na kumuua yeye na mwenzake wa Burundi, tukio ambalo lilichochea mauaji ya kimbari ya watu karibu milioni moja wengi wao wakiwa wa kabila la Tutsi.

Mauaji hayo yalifanywa na jeshi la zamani la Rwanda likishirikiana na wanamgambo wa kihutu wa Interahamwe.  

kimbari

Watu milioni moja waliuawa katika mauaji ya kimbari ya Rwanda

Mwendesha Mashtaka wa mahakama hiyo  Capt. Kayihura Kayijuka ameiambia mahakama kwamba, Jean Claude Seyoboka aliwapa mafunzo wanamghambo wa Interehamwe na kufanya mauaji dhidi ya Watutsi katika maeneo mbalimbali ya jiji la Kigali.

Seyoboka pia anatuhumiwa kwamba aliongoza shambulizi lililoua wanasiasa wawili wa zamani wa Rwanda, Theoneste Gafaranga na Andre Kameya ambao walipinga mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi.