Mahakama Nigeria yamnyima dhamana mkuu wa Biafra
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i20599-mahakama_nigeria_yamnyima_dhamana_mkuu_wa_biafra
Mahakama Kuu ya Nigeria imekataa kumuachia huru kwa dhamana mkuu wa harakati ya Biafra inayopigania kujitenga na Nigeria.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Dec 02, 2016 04:33 UTC
  • Mahakama Nigeria yamnyima dhamana mkuu wa Biafra

Mahakama Kuu ya Nigeria imekataa kumuachia huru kwa dhamana mkuu wa harakati ya Biafra inayopigania kujitenga na Nigeria.

Jaji wa mahakama kuu ya federali mjini Abuja Binta Nyako jana Alkhamisi alisema, tuhuma zinazomuandama Nnamdi Kanu, mkuu wa harakati ya kupigania kujitenga na Nigeria eneo la Biafra la kusini mwa nchi hiyo ni nzito na kwa msingi huo hawezi kupewa dhamana. Jaji huyo amebainisha kuwa, Kanu pamoja na washukiwa wengine watatu wanaweza kuhukumiwa vifungo vya maisha jela.

Rais Muhamadu Buhari wa Nigeria na Nnamdi Kanu, mkuu wa Biafra

Mwezi Februari mwaka huu, jaji mwengine wa mahakama hiyo John Tsoho vile vile alikataa maombi ya mawakili wa washukiwa hao, ya kuwaachia huru kwa dhamana wateja wao. Kanu ambaye alikamatwa mwezi Oktoba mwaka jana 2015, anakabiliwa na tuhuma za usaliti na uhaini kama wenzake watatu.

Haya yanajiri wiki moja baada ya Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International kusema wanaharakati wapatao 150 wa vuguvugu hilo linaloshinikiza kujitenga jimbo la Biafra wameuliwa na jeshi la Nigeria katika kipindi cha Agosti mwaka jana 2015 na Agosti mwaka huu.

Wafuasi wa harakati ya Biafra wakifanya maandamano

Hata hivyo Sani Usman, msemaji wa jeshi la Nigeria alikanusha ripoti hiyo na kuitaja kuwa ni ya upande mmoja na kusisitiza kuwa, askari watano waliuliwa na wanaharakati hao wakati wa maandamano ya mwezi Mei mwaka huu mbali na kushambuliwa magari ya jeshi na polisi.