Rais Dos Santos wa Angola kuachia ngazi mwaka 2017
(last modified Sat, 03 Dec 2016 14:20:51 GMT )
Dec 03, 2016 14:20 UTC
  • Rais  Dos Santos wa Angola kuachia ngazi mwaka 2017

Imedokezwa kuwa Rais Jose Eduardo dos Santos wa Angola, ambaye amekuwa madarakani tokea mwaka 1979, hatasimama tena katika uchaguzi wa rais utakaofanyika nchini humo mwakani.

Kwa mujibu wa waraka wa chama ambao haujatangazwa rasmi, inatazamiwa kuwa Waziri wa Ulinzi Joao Lourenco ambaye pia ni naibu mwenyekiti wa chama tawala cha MPLA' ameteuliwa kuwa  mrithi wa Dos Santos baada ya rais huyo kumpendekeza siku ya Alhamisi.

Chama cha MPLA siku ya Alhamisi kilikanusha uvumi uliokuwa umeenea katika mitandao ya kijamii kuwa Dos Santos anaugua.

Watu wa  Angola wamekuwa wakijadili mustakabali wa siasa nchini humo baada ya Dos Santos kutangaza mwezi Machi kuwa ataachia ngazi kabla ya mwaka 2018.

Uchaguzi wa bunge utafanyika  Agosti mwaka 2017 na kiongozi wa chama chenye idadi kubwa ya wabunge kuchukua nafasi ya urais wa nchi.

Kiongozi wa MPLA  Dos Santos, ambaye ni mhandisi wa mafuta, aliteuliwa kuwa rais kwa muhula mwingine wa miaka mitano mwaka 2012 baada ya chama chake kupata ushindi wa kishindo.

Angola ni mzalishaji mkubwa zaidi wa mafuta ya petroli Afrika na pia ni mwanachama wa nchi zinaozuza mafuta kwa wingi duniani OPEC lakini imekumbwa na matatizo ya kiuchumi kutokana na kuporomoka bei ya mafuta duniani.