Vikosi vya Somalia vyaua magaidi 7 wa ISIS
Wanajeshi wa Somalia wamefanikiwa kuwaua magaidi saba wanaofungamana na kundi la kigaidi la ISIS au Daesh katika mapigano yaliyojiri kaskazini mwa nchi hiyo siku ya Jumamosi.
Taarifa zinasema wanajeshi wa eneo lenye mamlaka ya ndani la Puntland walikabiliana na magaidi hao katika kijiji cha Bashaashin yapata kilomita 34 kutoka mji wa Bandari wa Qandala ambao ulitekwa na magaidi hao mapema mwezi Novemba.
Afisa wa ngazi za juu wa kijeshi Puntland Kapteni Mohamed Said amewaambia waandishi habari kuwa vikosi wa eneo hilo vimewaangamiza magaidi saba wa ISIS na kuchukua silaha walizokuwa nazo. Amesema oparesheni ya kuwasaka magaidi hao itaendelea hadi utakapokombolewa mji wa Qandala.
Idadi ya magaidi katika eneo hilo inakadiriwa kuwa mamia na wanaongozwa na Abdiqadir Mumin aliyejitenga na kundi la kigaidi la Al Shabab linalofungamana na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda.
Hayo yanajiri wakati ambao Umoja wa Mataifa umetoa wito kwa jumuiya za kitaifa kutoa misaada ya kibinadamu kwa Somalia kutokana na ukame wa muda mrefu nchini humo.
Ni karibu miaka 25 sasa ambapo Somalia inakabiliwa na vita vya ndani. Wanajeshi wa nchi za Kiafrika karibu elfu 22 wametumwa Somalia kupambana na al Shabab tangu mwaka 2007.