Uchaguzi wa Rais nchini Niger waingia duru ya pili
(last modified Sun, 28 Feb 2016 07:38:55 GMT )
Feb 28, 2016 07:38 UTC
  • Uchaguzi wa Rais nchini Niger waingia duru ya pili

Uchaguzi wa Rais nchini Niger uliofanyika Jumapili iliyopita na kuwapambanisha wagombea 15 umeingia duru ya pili baada ya kukosekana mshindi katika duru ya kwanza.

Tume Huru ya Uchaguzi ya Niger imetangaza kuwa, asilimia 67.46 ya wananchi wa nchi hiyo walishiriki katika duru ya kwanza ya uchaguzi huo. Katika duru ya kwanza ya uchaguzi, Rais wa sasa wa nchi hiyo Mahamadou Issoufou aliibuka wa kwanza kwa kujikusanyika zaidi ya asilimia 48. Hata hivyo kura hizo hazikutosha kumtangaza kuwa mshindi wa uchaguzi. Hama Amadou, Waziri Mkuu wa zamani wa Niger ambaye kwa sasa yuko jela alijipatia asilimia 17 ya kura na kushika nafasi ya pili. Uchaguzi huo umeingia duru ya pili katika hali ambayo, Rais Issoufou alikuwa na matumaini ya kushinda katika duru ya kwanza ya uchaguzi huo kutokana na kile kilichoelezwa kuwa kutokuweko mpinzani mkubwa wa kuweza kumkwamisha katika hilo. Hii ni katika hali ambayo, mrengo wa upinzani uliituhumu serikali kwamba, inapanga kuchakachua matokeo ya uchaguzi ili kiongozi wake aibuke mshindi katika duru ya kwanza tu ya uchaguzi huo. Hama Amadou ambaye sasa atachuana na Rais Mahamadou wa Niger katika duru ya pili ya uchaguzi, hana faili lenye kung'ara sana. Mwaka jana alitupwa jela kwa tuhuma za kujihusisha na magendo ya watoto.

Duru ya pili ya uchaguzi wa Rais nchini Niger imepangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi ujao wa Machi. Waangalizi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika ECOWAS wametangaza kuwa, licha ya kuweko matatizo na kasoro za hapa na pale, lakini kiujumla mazingira ya uchaguzi huo na jinsi zoezi lenyewe lililovyofanyika yalikuwa ya kuridhisha. Aidha waangalizi hao wamewataka wagombea pamoja na wananchi wa nchi hiyo kuheshimu matokeo ya uchaguzi.

Pamoja na hayo wananchi wa Niger wanaikosoa serikali kutokana na jinsi zoezi hilo la uchaguzi lilivyofanyika. Inaelezwa kuwa, vituo vingi vya kupigia kura vilifunguliwa kwa kuchelewa, huku baadhi ya vituo hivyo vikishindwa kupiga kura kabisa kutokana na kuchelewa vifaa vya kupigia kura kama vile makaratasi na masanduku ya kura.

Uchaguzi wa Rais nchini Niger unaingia duru ya pili katika hali ambayo, mashambulio ya wanachama wa kundi la kitakfiri na Boko Haram yangali yanaendelea katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.

Hivi karibuni ofisi ya masuala ya kibinaadamu ya Umoja wa Mataifa ilitangaza kuwa, zaidi ya Waniger milioni mbili wanahitajia msaada wa haraka wa chakula. Ukweli wa mambo ni kuwa, mwanasiasa yeyote atakayeibuka mshindi katika duru ya pili ya uchaguzi huo, atakuwa na kibarua kigumu cha kuivusha nchi hiyo katika hali yake mbaya ya hivi sasa kiuchumi.

Licha ya Niger kuwa na utajiri mkubwa wa madini muhimu ya urani, lakini nchi hiyo ambayo kijiografia ipo magharibi mwa Afrika inahesabiwa kuwa moja ya nchi maskini zaidi duniani.

Tags