Kanisa laporomoka na kuua watu zaidi ya 160 Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i21223-kanisa_laporomoka_na_kuua_watu_zaidi_ya_160_nigeria
Watu zaidi ya 160 wameuawa baada ya kanisa kuporomoka kusini mashariki mwa Nigeria Jumamosi.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Dec 11, 2016 11:14 UTC
  • Kanisa laporomoka na kuua watu zaidi ya 160 Nigeria

Watu zaidi ya 160 wameuawa baada ya kanisa kuporomoka kusini mashariki mwa Nigeria Jumamosi.

Habari zinasema kuwa, mkasa huo umetokea katika mji wa Uyo, makao makuu ya jimbo la Akwa Ibom mapema leo, wakati ambapo Wakristo walikuwa wamekusanyika kufanya ibada zao. Gavana wa jimbo hilo Udom Emmanuel, ambaye alikuwa katika kanisa hilo wakati wa mkasa, ameponea chupu chupu.

Mamlaka ya Kudhibiti Majanga nchini Nigeria NEMA imesema kuwa, kanisa hilo halikuwa limemalizwa kujengwa na yumkini hicho ndicho chanzo cha kuporokoma kwa paa lake, ingawaje maafisa usalama wameanzisha uchunguzi kubaini kiini hasa cha mkasa huo.

Ramani ya Nigeria

Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria ametuma mkono wa pole kwa familia, jamaa na marafiki wa wahanga wa ajali hiyo iliyosababisha mauaji ya makumi ya watu.

Duru za hospitali zinaarifu kuwa, huenda idadi ya walioaga dunia kutokana na mkasa huo ikaongezeka kutokana na hali mbaya ya majeruhi.

Si vibaya kukumbusha hapa kuwa, watu 116 walipoteza maisha baada ya jengo lililokuwa linamilikiwa na kanisa moja mjini Lagos kuporomoka mwaka 2014.

Wadadisi wa mambo wanaitakidi kuwa, visa hivi vya kuporomoka majengo nchini Nigeria, vimechangiwa na ufisadi, ambapo wanakandarasi na wakaguzi wa serikali wamekuwa wakiidhinisha ujenzi wa majengo bila kufuatilia na kutathmini vifaa na suhula zinazotumika, ambazo si za viwango vinavyostahili.