AU: Kuna wasiwasi wa magaidi kurejea barani Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i21454-au_kuna_wasiwasi_wa_magaidi_kurejea_barani_afrika
Kamisheni ya Amani na Usalama ya Umoja wa Afrika ina wasiwasi kwamba, kuna uwezekano maelfu ya magaidi wakarejea barani humo wakitokea Syria, Iraq na Yemen.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Dec 15, 2016 02:35 UTC
  • AU: Kuna wasiwasi wa magaidi kurejea barani Afrika

Kamisheni ya Amani na Usalama ya Umoja wa Afrika ina wasiwasi kwamba, kuna uwezekano maelfu ya magaidi wakarejea barani humo wakitokea Syria, Iraq na Yemen.

Kamishna wa Usalama na Amani wa Umoja wa Afrika, Ismail Chergui amesisitiza udharura wa nchi za Afrika kutilia maanani suala la ugaidi na ukosefu wa amani na kusema: Ripoti za kuaminika zinaonesha kuwa, baada ya magaidi kushindwa katika nchi za Syria, Iraq na Yemen sasa magaidi wapatao 2500 miongoni mwao wanaelekea katika ardhi ya Somalia.

Chergui ameeleza wasiwasi kuhusu ripoti za maelfu ya magaidi waliokuwa Syria, Yemen na Iraq kuelekea katika nchi za Ulaya na Afrika na kusema kuwa, kuna udharura wa kuwepo ushirikiano kati ya nchi za Afrika kwa ajili ya kupambana na ugaidi. Amesisitiza kuwa maeneo ya Pembe ya Afrika, Ziwa Chad na Sahel yanakabiliwa na tishio kubwa la usalama na amani.

Magaidi wa Daesh

Kamishna wa Amani na Usalama wa Umoja wa Afrika pia amezungumzia suala la kukombolewa mji wa Sirte kutoka mikononi mwa magaidi huko Libya na kusema maafisa wa Libya wanapaswa kuzidisha ulinzi katika maeneo ya mipaka ya nchi hiyo hususan mipaka ya majini.

Vilevile amezungumzia ushirikiano utakaoanza mwakani wa Polisi ya Afrika (Afripol) kwa lengo la kuzidisha udhibiti wa harakati za kigaidi na kusema kuwa ushirikiano huo utaanza baada ya kupasishwa na viongozi wa nchi za Afrika katika mkutano ujao wa viongozi hao.