AMISOM kuchunguza tuhuma za askari wake kuua raia Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i21805-amisom_kuchunguza_tuhuma_za_askari_wake_kuua_raia_somalia
Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) kimesema kimeanza uchunguzi kuhusu vifo vya raia sita vilivyotokea katika matukio tofauti huko Qoryooley mashariki mwa Somalia, mwishoni mwa wiki iliyopita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 20, 2016 11:26 UTC
  • AMISOM kuchunguza tuhuma za askari wake kuua raia Somalia

Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) kimesema kimeanza uchunguzi kuhusu vifo vya raia sita vilivyotokea katika matukio tofauti huko Qoryooley mashariki mwa Somalia, mwishoni mwa wiki iliyopita.

Umoja wa Afrika umesema ripoti za awali zinasema kuwa askari wa kikosi hicho walishambuliwa kwa makombora na watu wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa kundi la Al Shabaab.

AMISOM imesema, tuhuma zote zinazoelekezwa kwa askari wake zinachunguzwa kwa makini na hatua zinachukuliwa kufuata sheria na kanuni zinazoongoza kikosi hicho nchini Somalia.

Askari wa AMISOM wanatuhumiwa kushambulia basi lililokuwa limebeba raia katika wilaya ya Qoryoley yapata kilomita 120 kutoka mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Ujumbe wa Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM, umewahakikishia wananchi nchini humo kuhusu ahadi ya kufanya kazi na mamlaka za nchi kwa ajili ya kuwapatia ulinzi raia.

Kikosi cha AMISOM kina askari zaidi ya 20,000 wanaoisaidia serikali dhaifu ya Somalia kukabiliana na kundi la kigaidi la Al Shabab. Kikosi hicho cha AMISOM kinajumuisha askari kutoka nchi za Uganda, Ethiopia, Burundi, Djibouti, Kenya, na Sierra Leone.