Serikali ya DRC yawaachia huru wanaharakati wa upinzani
Polisi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imewaachia huru wanaharakati wa upinzani waliokamatwa hivi karibuni katika maandamano dhidi ya serikali ya Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo.
Ghislain Muhiwa, msemaji wa wanaharakati hao amethibitisha habari hiyo na kuongeza kuwa, wapinzani 19 waliokamatwa na polisi kwa madai ya kushiriki kinyume cha sheria maandamano dhidi ya serikali katika mji wa Goma, mashariki mwa nchi Disemba 21 wameachiwa huru. Amesema kuwa, mwanaharakati wa harakati ya upinzani ya Lucha, Gloria Senga, ambaye ilisemekana kutekwa nyara Disemba 18 mjini Kinshasa ni miongoni mwa wanaharakati hao19 walioachiwa huru.
Jose-Maria Aranaz, Mkurugenzi wa Ofisi ya Kutetea Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa Kongo DR amepongeza hatua hiyo ya vyombo vya dola ya kuwaachia huru wapinzani. Hata hivyo ameeleza wasi wasi wake kuhusu hatima ya wanachama wengine wa harakati ya upinzani ya Lucha ambao wangali wanazuiliwa na polisi ya nchi hiyo.
Ijumaa iliyopita, Umoja wa Mataifa ulisema kuwa, zaidi ya watu 40 wameuawa katika ghasia na maandamano ya wananchi ya kushinikiza Rais Kabila aachie ngazi, huku wengine 460 wakikamatwa na maafisa usalama kwa kushiriki maandamano hayo, yaliyopigwa marufuku na serikali ya Kinshasa.
Kwa mujibu wa katiba ya Kongo DR, Rais Joseph Kabila hastahiki kugombea kiti cha rais kwa mara nyingine baada ya kumalizika muhula wake wa uongozi mwezi huu wa Disemba, na hatua yake ya kutangaza kuwa atasalia madarakani hadi mwaka 2018 imechochea ghasia na maandamano katika miji mbali mbali nchini humo.