Wanigeria 3000 warejea katika makazi yao baada ya Boko Haram kutimuliwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i22339-wanigeria_3000_warejea_katika_makazi_yao_baada_ya_boko_haram_kutimuliwa
Wanigeria zaidi ya 3,000 wanaripotiwa kurejea katika makazi yao kaskazini mashariki mwa nchi baada ya magaidi wa Boko Harama kutimuliwa.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Dec 29, 2016 03:45 UTC
  • Wanigeria 3000 warejea katika makazi yao baada ya Boko Haram kutimuliwa

Wanigeria zaidi ya 3,000 wanaripotiwa kurejea katika makazi yao kaskazini mashariki mwa nchi baada ya magaidi wa Boko Harama kutimuliwa.

Jeshi la Nigeria limetoa taarifa likisema wakaazi wa mji wa Damasak ulio kaskazini magharibi mwa jimbo la Borno, ambalo limeathiriwa zaidi na ugaidi wa Boko Haram, wameanza kurejea katika nyumba zao. Eneo hilo, lenye ukubwa wa nchi ya Ubelgiji, lilitekwa na magaidi wa Boko Haram Disemba mwaka 2014 na magaidi kutimuliwa kutoka mji huo Julai mwaka huu.

Siku ya Jumamosi Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria alisema jeshi limechukua udhibiti wa msitu wa Sambisa katika jimbo hilo ambao ulikuwa ngome kuu ya Boko Haram.

Serikali imesema itafungua tena barabara mbili kutoka mji mkuu wa Borno, Maiduguri na miji ya Damasak na Baga kaskazini mwa jimbo hilo.

Magaidi wa Boko Haram

Tokea Boko Haram ianzishe uasi wake Nigeria mwaka 2009, watu zaidi ya elfu 20 wamepoteza maisha kutokana na hujuma za kundi hilo la magaidi wakufurishaji nchini Nigeria na pia katika nchi hiyo na nchi jirani za Cameroon, Niger na Chad. Aidha zaidi ya watu milioni mbili wamefanywa wakimbizi kufuatia ugaidi wa Boko Haram.

Neno Boko Haram kwa lugha ya Kihausa lina maana ya 'elimu kutoka nchi za Magharibi ni haramu'. Kundi hilo la Boko Haram ambalo lina ufahamu usio sahihi na potovu kuhusu dini ya Kiislamu, limekuwa likitekeleza hujuma katika maeneo mbalimbali ya Nigeria hasa kaskazini mwa nchi hiyo.