Watu 7 wauawa katika mapigano makali Afgoye, Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i22426-watu_7_wauawa_katika_mapigano_makali_afgoye_somalia
Watu saba wameuawa katika mapigano makali baina ya jeshi la Somalia na magaidi wa kundi la Al-Shabaab baada ya wapiganaji hao kushambulia kituo cha upekuzi cha jeshi mjini Afgoye, kilomita 30 kusini mwa Mogadishu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 30, 2016 11:57 UTC
  • Watu 7 wauawa katika mapigano makali Afgoye, Somalia

Watu saba wameuawa katika mapigano makali baina ya jeshi la Somalia na magaidi wa kundi la Al-Shabaab baada ya wapiganaji hao kushambulia kituo cha upekuzi cha jeshi mjini Afgoye, kilomita 30 kusini mwa Mogadishu.

Idara ya Upelelezi na Usalama ya Somalia imetangaza kuwa waliouawa ni askari watatu wa jeshi la Somalia na magaidi wanne.

Lakini gavana wa jimbo la Lower Shabelle Ibrahim Aden Ali amekanusha taarifa za kuuawa kwa askari hao na kusema askari hao wamejeruhiwa.

Nalo kundi la Al-Shabaab limedai, wapiganaji wake wamewaua baadhi ya wanajeshi na kudhibiti mji huo.

Ni karibu miaka 25 sasa ambapo Somalia haina serikali kuu tangu alipopinduliwa dikteta Muhammed Siad Barre mwaka 1991. Tangu wakati huo machafuko yameikumba nchi hiyo ya Pembe ya Afrika na kuziathiri pia nchi jirani ikiwemo Kenya. 

Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia kina askari zaidi ya 20,000 wanaoisaidia serikali dhaifu ya Mogadishu kukabiliana na kundi la kigaidi la Al Shabab. Kikosi hicho cha AMISOM kinajumuisha askari kutoka nchi za Uganda, Ethiopia, Burundi, Djibouti, Kenya, na Sierra Leone.