Jan 02, 2017 06:46 UTC
  • Qur'ani tukufu yatarjumiwa kwa lugha ya Kiyao, Malawi

Qur'ani Tukufu iliyotarjumiwa kwa lugha ya Kiyao ilizinduliwa Jumamosi iliyopita nchini Malawi.

Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa (IQNA) limeripoti kuwa, Qur'ani hiyo imezinduliwa na Jumuiya ya Waislamu Malawi (MAM) na Baraza la Iftaa la Mualmaa la Malawi katika mji wa Mangochi kusini mwa nchi hiyo.

Sheikh Muhammad Abdul-Hamid Silika ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Iftaa la Maulamaa wa Malawi ametumia muda wa miaka 10 kuitarjumu Qur'ani kwa lugha ya Kiyao.

Aidha tarjuma hiyo imepitiwa kwa muda wa miezi sita na jopo la maulamaa 14.

Rais wa zamani wa Malawi Bakili Muluzi amekuwa mtu kwa kwanza kununua nakala 200 za Qur'ani kwa lugha ya Yao na kuzitoa zawadi kwa wanawake waliohudhuria sherehe za uzinduzi huo.

Baadhi ya Waislamu waliohudhuria uzinduzi wa tarjumi ya Qur'ani kwa lugha ya Kiyao, Malawi

Akizungumza katika uzinduzi huo, Kaimu Mwenyekiti wa chama cha Peoples Part Uladi Mussa amesema tarjuma hiyo itawasaidia Waislamu ambao lugha yao asili ni Kiyao kuijua Qur'ani Tukufu na Uislamu.

Uladi Mussa amesema karibu asilimia 60-70 ya Waislamu wa Malawi ni Wayao na hivyo ni muhimu Qur'ani Tukufu kutarjumiwa kwa lugha wanayoifahamu kwa urahisi. 

Mwanasiasa hiyo pia ametoa wito kwa watu wa Malawi kuweka kando tafauti zao za kidini na kuelekeze nguvu zao katika ujenzi wa nchi na kuwekeza zaidi katika elimu.

 

Tags