Jan 04, 2017 07:30 UTC
  • Besigye atoa masharti ya kufanya mazungumzo na Rais Museveni

Kinara wa upinzani nchini Uganda ametoa masharti matano kwa serikali ya Rais Yoweri Museveni iwapo inataka kufanya mazungumzo ya kitaifa kuhusu mustakabali wa kisiasa wa nchi hiyo.

Dakta Kizza Besigye amesema sharti la kwanza ni kuwepo mpatanishi wa kigeni mwenye uwezo wa kuhakikisha kuwa makubaliano yote yatakayofikiwa kwenye mazungumzo hayo ya kitaifa yanatekelezwa na pande zote husika.

Masharti mengine aliyoyatoa kiongozi wa upinzani nchini Uganda ni kuweko ajenda iliyo wazi ya kufanyika mazungumzo hayo, kuandaliwa fremu rasmi ya mazungumzo hayo, kuundwa ramani ya njia ya kuhakikisha kuwa mapendekezo yote ya mazungumzo hayo yanatekelezwa na kuhakikisha kuwa mazungumzo hayo yanafanyika chini ya anga ya usawa na wala hakuna upande utakaojihisi kuwa bora katika mazungumzo hayo. 

Rais Yoweri Museveni wa Uganda

Hivi sasa Besigye anakabiliwa na kesi ya uhaini kwa kujitangaza mshindi wa uchaguzi wa mwaka jana na hata kujiapisha na kisha kusambaza kanda hiyo ya video katika mitandao ya kijamii. Alidai kuwa alipata asilimia 52 ya kura zilizopigwa katika uchaguzi huo.

Mabaraza ya Wazee na viongozi wa kidini nchini Uganda yamekuwa yakishinikiza kufanyika mazungumzo ya kitaifa nchini humo ili kupunguza joto la kisiasa sambamba na kuhamasisha utangamano miongoni mwa wananchi pasina kujali mirengo yao ya kisiasa.

Tags