Wapinzani wa kupewa Saudia visiwa viwili vya Misri waja juu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i23038-wapinzani_wa_kupewa_saudia_visiwa_viwili_vya_misri_waja_juu
Wapinzani wa mpango wa serikali ya Misri wa kutaka kuipa Saudi Arabia visiwa viwili vya Tiran na Sanafir vya Bahari Nyekundu wamezidi kuonesha hasira zao na wameipa Cairo muda maalumu kuhakikisha imeachana na mpango wake huo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 07, 2017 23:43 UTC
  • Wapinzani wa kupewa Saudia visiwa viwili vya Misri waja juu

Wapinzani wa mpango wa serikali ya Misri wa kutaka kuipa Saudi Arabia visiwa viwili vya Tiran na Sanafir vya Bahari Nyekundu wamezidi kuonesha hasira zao na wameipa Cairo muda maalumu kuhakikisha imeachana na mpango wake huo.

Shirika la habari la Fars limeripoti kuwa, vyama na mirengo ya kisiasa inayopinga mpango wa kuchorwa upya mpaka wa baharini baina ya Saudia na Misri na kupewa Saudi Arabia visiwa hivyo viwili vya Misri, ilisema jana kuwa, Jumatano ijayo wataandamana mbele ya jengo la Waziri Mkuu wa Misri kutangaza upinzani wao kuhusu mpango huo.

Vyama na mirengo hiyo ya kisiasa imekubaliana kufanya mazungumzo na waandishi wa habari katika makao makuu ya chama cha al Karamah ili kutoa ufafanuzi kuhusu maandamano yao mbele ya jengo la Waziri Mkuu pamoja na maandamano kama hayo yanayotarajiwa kufanyika tarehe 16 mwezi huu wa Januari ili kuishinikiza serikali ya Misri iachane na mpango wake huo.

Wananchi wa Misri wakiandamana kupinga mpango wa serikali ya Abdul Fattah el Sisi wa kutaka kuupa ukoo wa Aal Saud wa Saudia visiwa viwili vya Misri

 

Katibu Mkuu wa chama cha al Karamah amesema, kuna hati na tangazo maalumu limeandaliwa ili kuzitahadharisha taasisi husika na tangazo hilo litatolewa masaa 72 kabla ya kufanyika maandamano ya kupinga mpango huo. Iwapo taasisi husika hazitaitikia mwito huo, basi wananchi watafanya maandamano makubwa nchini Misri.

Itakumbukwa kuwa wiki iliyopita, mahakama ya rufaa ya Misri ilikubaliana na rufaa iliyokatwa na serikali ya nchi hiyo na kuruhusu kupewa ukoo wa Aal Saud wa Saudi Arabia, visiwa viwili vya Misri vya Tiran na Sanafir. Wananchi wengi wa Misri wanalalamika kuwa viongozi wa serikali ya Cairo wameamua kuuza ardhi ya Misri kwa manufaa yao binafsi.