UN yataka ushirikiano chanya katika mapambano dhidi ya Boko Haram
Umoja wa Mataifa umetaka kuzidishwa ushirikiano kati ya nchi za eneo la Ziwa Chad katika mapambano dhidi ya kundi la kigaidi la Boko Haram.
Taye-Brook Zerihoun Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya kisiasa ameashiria kuongezeka jitihada za kijeshi katika eneo la Ziwa Chad kwa ajili ya kuliangamiza kundi la kigaidi la Boko Haram na kueleza kuwa kundi hilo lingali lina uwezo wa kutekeleza oparesheni za kigaidi.
Zerihoun aliyasema hayo jana katika kikao cha nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya kisiasa amesisitiza kuwa kundi la kigaidi la Boko Haram limepoteza baadhi ya maeneo yaliyokuwa mikononi mwake, hata hivyo akasema kundi hilo linasalia kuwa tishio kwa usalama wa eneo na kwamba, nchi za eneo la Ziwa Chad zinapasa kuimarisha stratejia yao ya vita vya pamoja dhidi ya kundi hilo.
Naye stephen O'Brien Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya kibinadamu ametahadharisha kuhusu kuongezeka maafa ya kibinadamu huko kaskazini mashariki mwa Nigeria, katika baadhi ya maeneo ya Cameroon, Chad na Niger.