Nchi za Afrika Magharibi kumuondoa Jammeh madarakani kwa nguvu, Gambia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i23752-nchi_za_afrika_magharibi_kumuondoa_jammeh_madarakani_kwa_nguvu_gambia
Nigeria na nchi kadhaa za Afrika Magharibi zinapanga kutuma majeshi nchini Gambia kumuondoa madarakani Rais Yahya Jammeh iwapo hatakabidhi madaraka kama ilivyopangwa.
(last modified 2025-11-07T02:31:33+00:00 )
Jan 17, 2017 15:10 UTC
  • Nchi za Afrika Magharibi kumuondoa Jammeh madarakani kwa nguvu, Gambia

Nigeria na nchi kadhaa za Afrika Magharibi zinapanga kutuma majeshi nchini Gambia kumuondoa madarakani Rais Yahya Jammeh iwapo hatakabidhi madaraka kama ilivyopangwa.

Duru za jeshi la Nigeria zimedokeza kuwa, "Uamuzi umeshachukuliwa kwamba, Jammeh hatabakia kuwa rais wa Gambia baada ya kumalizika muhula wake."

Jammeh alishindwa katika uchaguzi uliofanyika Disemba mosi ambapo mpinzani wake mkuu, Adama Barrow alipata ushindi na anatazamiwa kuapishwa Alhamisi ijayo. Awali Jammeh alikubali kushindwa lakini baada ya hapo akabatilisha uamuzi wake huo kwa madai kuwa kulifanyika wizi wa kura katika uchaguzi huo.

Hivi karibuni Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa Afrika Magharibi Mohamed Ibn Chambas alisema ikiwa ushawishi utashindikana kuna mpango wa kutumia kila mbinu ikiwemo ya matumizi ya nguvu kuhakikisha matakwa ya watu wa Gambia yanatimizwa. Alisema ikiwa kutahitajika nguvu za kijeshi kumuondoa Jammeh madarakani, ECOWAS inatarajia kusaka ridhaa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Afrika ili kutuma vikosi vya jeshi huko Gambia.'

Adama Barrow

Hivi sasa Barrow yuko katika nchi jirani ya Senegal kufuatia uamuzi uliochukuliwa na viongozi wa  ECOWAS waliokutana nchini Mali siku kadhaa zilizopita.

Hii ni baada ya Rais Yahya Jammeh kuendelea kung'ang'ania madaraka akisisitiza kuwa uamuzi wa mwisho wa kadhia hiyo utatolewa na mahakama.