Morocco yaazimia kurejea katika Umoja wa Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i23899-morocco_yaazimia_kurejea_katika_umoja_wa_afrika
Bunge la Morocco limepiga hatua moja mbele ikiwa ni juhudi za nchi hiyo kutaka kurejea katika Umoja wa Afrika baada ya kujiondoa kwa zaidi ya miongo mitatu iliyopita.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 19, 2017 14:08 UTC
  • Morocco yaazimia kurejea katika Umoja wa Afrika

Bunge la Morocco limepiga hatua moja mbele ikiwa ni juhudi za nchi hiyo kutaka kurejea katika Umoja wa Afrika baada ya kujiondoa kwa zaidi ya miongo mitatu iliyopita.

Mapema leo Wabunge 395 wa Morocco walipasisha muswada wa nchi yao kurejea tena katika Umoja wa Afrika. Uamuzi huo wa Bunge la Morocco umetajwa kuwa ni hatua moja mbele ya mchakato wa nchi hiyo kurejea tena katika Umoja wa Afrika.

Hatua hiyo ya Bunge la Morocco imekuja miezi kadhaa baada ya Mfalme Mohammed wa VI wa nchi hiyo kutangaza wazi azma ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika ya kutaka kurejea katika Umoja wa Afrika AU, baada ya kuondoka katika umoja huo zaidi ya miongo mitatu iliyopita.

Mfalme wa Morocco alipoitembelea Tanzania Oktoba 2016

Ikumbukwe kuwa, Morocco inanufaika na huduma zinazotolewa kwa nchi zote wanachama wa AU, lakini wakati huo huo inasalia kuwa nchi pekee ya Kiafrika mwanachama wa Umoja wa Mataifa ambayo si mwanachama wa Umoja wa Afrika. Morocco iliamua kujiondoa katika Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) wakati huo mwaka 1984 kufuatia uamuzi wa umoja huo wa kuafiki uanachama wa Jamhuri ya Sahara Magharibi iliyojitangaza kuwa huru. Morocco inaihesabu jamhuri hiyo kuwa ni sehemu ya ardhi yake.

Mwezi Oktoba mwaka jana, Mfalme Mohammed wa VI wa Morocco alifanya ziara katika nchi tatu za Afrika Mashariki ambayo ilitajwa kuwa na lengo la kutafuta uungaji mkono wa kurejea nchi hiyo kuwa mwananchama wa Umoja wa Afrika, baada ya kujiondoa kwenye umoja huo miaka 33 iliyopita.