Pigo jingine kwa wanamgambo wa al Shabab nchini Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i24028-pigo_jingine_kwa_wanamgambo_wa_al_shabab_nchini_somalia
Jeshi la Somalia limetangaza kuwa, wanamgambo wasiopungua sita wa al Shabab wameuawa katika operesheni ya jeshi hilo kusini mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 21, 2017 10:19 UTC
  • Pigo jingine kwa wanamgambo wa al Shabab nchini Somalia

Jeshi la Somalia limetangaza kuwa, wanamgambo wasiopungua sita wa al Shabab wameuawa katika operesheni ya jeshi hilo kusini mwa nchi hiyo.

Jeshi hilo limenukuliwa na vyombo vya habari likitangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, jeshi la Somalia kwa kushirikiana na kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika AMISOM vimeendesha operesheni maalumu ya kukabiliana na wanamgambo wa al Shabab na kufanikiwa kuua wanamgambo sita. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wanajeshi wawili wa serikali wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa kwenye operesheni hiyo iliyofanyika katika eneo la Afgooye, la kusini mwa Somalia.

Kabla ya hapo Muhammad Ibrahim Abdullah, afisa wa ngazi za juu wa masuala ya usalama wa Somalia alikuwa amesema kuwa, Abdi Adan, kamanda wa ngazi za juu wa al Shabab ameangamizwa katika opereseheni maalumu ya jeshi la Somalia kwenye eneo la Hiran, katikati ya Somalia.

Askari wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika AMISOM wakiwa katika operesheni ya kupambana na al Shabab huko Afgooye, kusini mwa Somalia

 

Tangu mwaka 2012, kundi la kigaidi la al Shabab ambalo ni sehemu ya mtandao wa kigaidi wa al Qaida liliteka baadhi ya maeneo ya kusini na katikati mwa Somalia. Hata hivyo mwaka juzi yaani 2015 lilipoteza miji yote mikubwa na hivi sasa limebakia katika baadhi tu ya maeneo ya vijijini.

Mwaka 2014 idadi ya wapiganaji wa al Shabab walikadiriwa kuwa ni baina ya elfu saba hadi tisa.