Magaidi wa al-Shabab washambulia Lower Shebelle, Somalia 5 wauawa
Wanachama wa kundi la kigaidi la al-Shabab nchini Somalia wamefanya shambulizi eneo la Lower Shebelle na kuua watu watano.
Abdul-Rahman Ahmed, kamanda wa jeshi la Somalia amethibitisha habari hiyo na kusema kuwa, shambulizi hilo limeandana na hujuma ya ufyatuaji risasi wa wanachama wa genge hilo kusini mwa mji mkuu wa nchi hiyo, Mogadishu na kwamba watu wengine kadhaa wamejeruhiwa. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, idadi ya wahanga itaongezeka kutokana na hali ya baadhi ya majeruhi kuwa mbaya.
Weledi wa mambo wameitaja hujuma hiyo kama zoezi la kulipiza kisasi kufuatia mafanikio ya jeshi la Somalia katika operesheni zake za hivi karibuni ambazo siku chache zilizopita zilipelekea wanamgambo kadhaa wa al-Shabab kuuawa na wengine kujeruhiwa.
Hivi karibuni jeshi hilo lilitangaza kuwa, jeshi la Somalia kwa kushirikiana na kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika, AMISOM limefanya operesheni maalumu ya kukabiliana na wanamgambo wa al-Shabab na kufanikiwa kuua wanamgambo wengine wa genge hilo.
Kundi la kigaidi la al-Shabab limekuwa likiendesha harakati zake nchini Somalia tangu mwaka 2007 kwa lengo la kuing'oa serikali ya nchi hiyo. Mwaka 2011 kundi hilo lilifanikiwa kudibiti mji mkuu wa Somalia, Mogadishu na Afgooye. Hata hivyo operesheni za jeshi la nchi hiyo kwa kushirikiana na askari wa AMISOM zilifanikisha kuwatimua wanachama wa kundi hilo kutoka maeneo hayo.