Umoja wa Afrika wataka askari 4,000 zaidi watumwe Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i24339-umoja_wa_afrika_wataka_askari_4_000_zaidi_watumwe_somalia
Umoja wa Afrika AU umetoa wito wa kuongezwa idadi ya askari wanaohudumu chini ya mwavuli wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jan 27, 2017 23:19 UTC
  • Umoja wa Afrika wataka askari 4,000 zaidi watumwe Somalia

Umoja wa Afrika AU umetoa wito wa kuongezwa idadi ya askari wanaohudumu chini ya mwavuli wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM.

Katika mkutano wake wa 22 katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, Kamati ya Kuratibu Operesheni za Kijeshi ya Umoja wa Afrika imesema kuwa, kuna haja Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa kwa ujumla kuunga mkono mpango huo wa kutumwa wanajeshi elfu 4 zaidi wa kieneo nchini Somalia.

Taarifa ya kamati hiyo imekariri wito wa kuendelea kulisaidia Jeshi la Taifa la Somalia, ili liweze kulitokomeza kundi la kigaidi la al-Shabaab, ambalo limevuruga usalama na uthabiti wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Askari wa Amisom wakishika doria nchini Somalia

Kamisheni ya AU inatazamiwa kuandaa mkutano mwingine kuhusu kadhia ya Somalia kabla ya kumalizika mwezi Februari, ambao utawaleta pamoja wawakilishi wa Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya, Jeshi la Taifa la Somalia na nchi wafadhili wa kikosi cha AMISOM, Marekani na Uingereza. 

Askari wa Umoja wa Afrika nchini Somalia wamepata mafanikio ya kiwango fulani ikiwa ni pamoja na kurejesha usalama katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo, ingawa wanamgambo wa genge la al-Shabaab wamekuwa wakifanya hujuma za hapa na pale ndani ya miji tofauti ya nchi hiyo. 

Kikosi cha AMISOM kina askari zaidi ya 20,000 wanaoisaidia serikali dhaifu ya Somalia kukabiliana na kundi la kigaidi la al-Shabaab, kikiwa na askari kutoka Uganda, Ethiopia, Burundi, Djibouti, Kenya, na Sierra Leone.