Muungano wa Mabunge ya Kiislamu wasisitiza himaya yake kwa taifa la Palestina
Washiriki wa mkutano wa Muungano wa Mabunge ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC wamesisitiza juu ya udharura wa kuungwa mkono na kutetewa taifa la Palestina mkabala na uvamizi wa utawala haramu wa Israel.
Washiriki wa mkutano huo wa 12 wa Muungano wa Mabunge ya Kiislamu uliofanyika mjini Bamako, mji mkuu wa Mali jana walitoa taarifa yao mwishoni mwa mkutano wao na kutoa wito wa kufanyika juhudi za duru za kieneo na kimataifa kwa ajili ya kuhakikisha Wapalestina wanapatiwa haki zao za kisheria hususan haki ya kurejea makwao wakimbizi wa Kipalestina, kukombolewa maeneo yote ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na kuundwa nchi huru ya Palestina mji mkuu wake ukiwa Baytul Muqaddas.
Sehemu nyingine ya taarifa ya mwisho ya mkutano wa Muungano wa Mabunge ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC imesema kuwa, hatua ya Marekani ya kutaka kuuhamishia ubalozi wake mjini Baytul Muqaddas kutoka Tel Aviv si ya kisheria na kwamba, huo ni uadui wa wazi dhidi ya Wapalestina na haki zao.
Aidha washiriki wa mkutano wa Muungano wa Mabunge ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC wametaka kuondolewa mzingiro wa kidhulma dhidi ya taifa la Palestina, kuachiliwa huru mateka wa Kipalestina na kupandishwa kizimbani viongozi wa utawala haramu wa Israel kutokana na kutenda kwao jinai dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.