Viongozi wa Afrika waafiki stratejia ya kujiondoa ICC kwa pamoja?
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i24547-viongozi_wa_afrika_waafiki_stratejia_ya_kujiondoa_icc_kwa_pamoja
Viongozi wa Afrika wameunga mkono stratejia inayotaka nchi za bara hilo zijiondoe katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kwa pamoja.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Feb 01, 2017 04:15 UTC
  • Viongozi wa Afrika waafiki stratejia ya kujiondoa ICC kwa pamoja?

Viongozi wa Afrika wameunga mkono stratejia inayotaka nchi za bara hilo zijiondoe katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kwa pamoja.

Uamuzi huo ambao unazipa nchi za bara hilo khiari ya kuamua iwapo zinataka kujiondoa kwa pamoja au la, ulifikiwa jana katika mazungumzo ya faragha pambizoni mwa mkutano wa Umoja wa Afrika katika makao makuu ya AU huko Addis Ababa, Ethiopia.

Duru za karibu na mkutano huo zinaarifu kuwa, kulikuwa na mgawanyiko mkubwa kwenye mazungumzo hayo ya faragha kileleni mwa mkutano wa AU, baadhi ya nchi zikiunga mkono wazo hilo la kujiondoa kwa pamoja huku zingine zikishikilia kuwa kila nchi ijiondoe kivyake.

Elise Keppler, afisa wa shirika la kutetea haki za binadamu Human Rights Watch amesema stratejia hiyo haina muda maalumu wa utekelezwaji, wala haina mapendekezo madhubuti.

Jengo la mahakama ya ICC mjini The Hague, Uholanzi

Hii ni katika hali ambayo, siku chache kabla ya kuanza mkutano wa AU, Nigeria ilisema haiungi mkono pendekezo hilo linalotaka nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kujiondoa ICC kwa pamoja. Geoffrey Onyeama, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Nigeria alisema, Zambia, Tanzania, Liberia na Botswana huko nyuma zilitangaza msimamo wao wa kutojiondoa kwenye Mkataba wa Roma uliounda ICC na hivyo haingii akilini kuzilazimisha nchi zote wanachama wa Umoja wa Afrika kujiondoa kwa pamoja.

Tayari Gambia, Afrika Kusini na Burundi zimeanzisha mchakato wa kujiondoa katika Mkataba wa Roma kutokana na kile viongozi wa nchi hizo sawa na viongozi wengine wa Kiafrika wanakitaja kuwa, ICC kuwasakama tu viongozi wa nchi za bara hilo, huku ikifumbia macho jinai zinazofanywa na viongozi wa Magharibi.