Maonesho ya kwanza maalumu ya Iran Afrika Mashariki kufunguliwa Nairobi, Kenya
Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Kenya amesema, maonyesho ya kwanza maalumu ya Iran katika Afrika Mashariki katika nyuga za utaalamu wa ujenzi, mawasiliano na teknolojia, petroli na gesi, petrokemikali, teknolojia ya viumbe hai na tiba yatafunguliwa siku ya Ijumaa katika mji mkuu wa nchi hiyo Nairobi.
Hadi Farajvand, amebainisha kuwa mashirika 120 ya Kiirani yataonyesha na kutangaza bidhaa zao za ujenzi, mawasiliano na teknolojioa, mafuta na gesi, petrokemikali, teknolojia ya viumbe hai, tiba, dawa, mabusati, vifaa vya nyumbani pamoja na bidhaa za vyakula na nguo katika maonyesho hayo ya kwanza maalumu ya Iran katika Afrika Mashariki yatakayoanza Ijumaa ya tarehe 3 Februari mjini Nairobi.
Balozi wa Iran mjini Nairobi amebainisha kuwa maonyesho hayo yamepokelewa kwa hamu kubwa na ni mwanzo wa maelewano na kustawishwa uhusiano wa kiuchumi na kibiashara wa Iran na Kenya.
Maonyesho hayo yatakayoendelea kwa muda wa siku nne, yanatazamiwa kufunguliwa na Mojtaba Khosrutaj, Mkuu wa Shirika la Ustawi wa Biashara la Iran katika hafla itakayohudhuriwa na viongozi wa Kenya pamoja na baadhi ya mabalozi na wanadiplomasia wa kigeni walioko nchini humo…/