Wahajiri wengine 120 wa Kiafrika waokolewa katika pwani ya Libya
(last modified Sun, 05 Feb 2017 14:17:21 GMT )
Feb 05, 2017 14:17 UTC
  • Wahajiri wengine 120 wa Kiafrika waokolewa katika pwani ya Libya

Kikosi cha ulinzi katika pwani ya Libya kimearifu kuwa wahajiri zaidi ya 120 wameokolewa majini karibu na bandari ya Tripoli kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.

Shirika la habari la Ufaransa limeripoti kuwa wahajiri wa Kiafrika ambao juzi Ijumaa waliondoka kwa boti katika mji wa kale wa Sabratah umbali wa kilomita 70 magharibi mwa Tripoli mji mkuu wa Libya kwa lengo la kuingia Ulaya, boti yao ilipatwa na ajali wakiwa safarini. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, askari wa doria wanaolinda pwani ya Libya leo wamefanikiwa kuwaokoa wahajiri hao umbali wa maili 20 kaskazini mashariki mwa mji mkuu wa Libya Tripoli. Wahajiri hao ambao wametajwa kuwa ni wenye asili ya Kiafrika ambapo miongoni mwao kumeshuhudiwa wanawake kumi na watoto watano, wamepelekwa katika bandari moja mashariki mwa mji mkuu wa Libya Tripoli.

Wahajiri wa Kiafrika waliopata ajali ya boti na kuokolewa katika pwani ya Libya

Kikosi cha ulinzi katika pwani ya Libya jana pia kilitangaza kuwa siku kadhaa zilizopita kiliwazuia wahajiri zaidi ya 4000 kuelekea Ulaya. Libya imekuwa katika hali ya mchafukoge na ukosefu wa amani tangu mwaka 2011 baada ya Muungano wa kijeshi wa nchi za Magharibi Nato kuingilia kijeshi huko Libya na kumng'oa madarakani dikteta wa nchi hiyo Muammar Gaddafi. Nchi hiyo pia imegeuzwa kuwa mahala pa kufanyia biashara ya magendo ya wahajiri wanaoelekea barani Ulaya. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, katika mwaka huu wa 2017, wahajiri karibu 230 wameaga dunia wakiwa njiani kuelekea katika nchi za Ulaya.

Tags