Feb 08, 2017 07:28 UTC
  • Kiongozi wa kaskazini mwa CAR aitaka serikali kudhamini usalama wa Bocaranga

Mwakilishi wa mji wa Bocaranga, kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati ameitaka serikali ya nchi hiyo kudhamini usalama wa eneo hilo la mpakani kutokana na hujuma za makundi ya wabeba silaha.

Anicet Georges Dologuélé, sanjari na kusisitizia suala hilo ameonyesha masikitiko yake kutokana na mauaji ya hivi karibuni dhidi ya raia wa kawaida kufuatia mapigano baina ya makundi ya wabeba silaha wa Anti-Balaka na wale wa Seleka. Kwa mujibu wa Dologuélé katika hujuma hiyo, wapiganaji wa makundi hayo walipora pia mali za raia.

Magaidi wa kundi la Kikristo la Anti-Balaka nchini CAR

Naye kwa upande wake, Jean pierre Guerret-Pidoux, kiongozi wa chama cha kisiasa cha Harakati kwa ajili ya Ukamilifu wa Kijamii (MES) amesema kuwa, kushadidi mapigano nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, kunatokana na kubadilika kwa siasa za serikali ya sasa licha ya kuwepo askari wengi wa kusimamia amani wa Umoja wa Mataifa. Itafahamika kuwa, mapigano nchini humo yaliibuka tena miezi michache iliyopita na kupelekea maelfu ya raia kuwa wakimbizi.

Rais Faustin-Archange Touadéra wa CAR

Weledi wengi wa masuala ya kisiasa walitaraji kwamba, kuingia madarakani Rais Faustin-Archange Touadéra kungeboresha hali ya kisiasa na utulivu nchini, lakini kuendelea kusalia silaha katika mikono ya makundi ya waasi kumeharibu zaidi hali ya mambo nchini humo.

Tags