Ash-Shabab washambulia uwanja wa ndege wa Mogadishu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i24861-ash_shabab_washambulia_uwanja_wa_ndege_wa_mogadishu
Kundi la kigaidi na kitakfiri la ash-Shabab nchini Somalia, limeshambulia uwanja wa ndege wa Mogadishu, mji mkuu wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 08, 2017 04:17 UTC
  • Ash-Shabab washambulia uwanja wa ndege wa Mogadishu

Kundi la kigaidi na kitakfiri la ash-Shabab nchini Somalia, limeshambulia uwanja wa ndege wa Mogadishu, mji mkuu wa nchi hiyo.

Ash-Shabab wametekeleza shambulizi hilo kwa makombora, licha ya kushadidishwa usalama na ulinzi mjini hapo kwa mnasaba wa uchaguzi wa rais unaofanyika leo nchini humo. Kwa mujibu wa mashuhuda, katika hujuma hiyo kundi hilo limedhibiti pia kambi ya kijeshi ya askari wa Umoja wa Afrika iliyo umbali wa kilometa 25 katika mji mkuu huo.

Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud

Hii ni katika hali ambayo Jumatatu iliyopita kundi hilo liliwanyonga raia wanne kwa tuhuma za kufanya ujasusi kwa ajili ya serikali ya Somalia, Marekani na Kenya. Uchaguzi wa rais nchini Somalia unafanyika leo katka hali ambayo awali ulikuwa umeakhirishwa mara tano mfululizo kutokana na ukosefu wa usalama.

Askari wa Somalia wakiimarisha usalama nchini 

Jumla ya wagombea 22 wanachuana kuwania nafasi hiyo. Aidha jumla ya wabunge 275 na pia maseneta 54 wa nchi hiyo watamchagua rais wa Somalia katika uwanja wa ndege wa Mogadishu. Shambulizi la wanachama wa genge hilo la kigaidi limetekelezwa kwa lengo la kukwamisha zoezi hilo muhimu dhidi ya serikali ya Rais Hassan Sheikh Mohamud wa nchi hiyo.