UN: Wakimbizi 52,000 wa Sudan Kusini wameingia Uganda mwezi jana
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i24905-un_wakimbizi_52_000_wa_sudan_kusini_wameingia_uganda_mwezi_jana
Umoja wa Mataifa umesema wakimbizi 52,000 raia wa Sudan Kusini waliingia nchini Uganda mwezi uliopita pekee wa Januari, kutokana na kuendelea kushuhudiwa mauaji na machafuko katika nchi yao.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Feb 09, 2017 03:56 UTC
  • UN: Wakimbizi 52,000 wa Sudan Kusini wameingia Uganda mwezi jana

Umoja wa Mataifa umesema wakimbizi 52,000 raia wa Sudan Kusini waliingia nchini Uganda mwezi uliopita pekee wa Januari, kutokana na kuendelea kushuhudiwa mauaji na machafuko katika nchi yao.

Adama Dieng, Mjumbe Maalumu wa UN katika masuala ya kukabiliana na mauaji ya kimbari amesema kuwa, aghalabu ya wakimbizi hao waliokimbilia Uganda wamesema walilazimika kutoroka nchi kutokana na kushadidi mauaji, ubakaji na jinai nyingine za kutisha hususan kusini mwa mji mkuu Juba, jimbo la Central Equatoria.

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, watu wanauawa kwa umati na kutendewa jinai nyinginezo za kutisha katika eneo la Kajo-Keji. Hata hivyo ameongeza kuwa, yumkini hali hiyo itabadilika baada ya kikosi cha askari wa UN kuwasili katika eneo hilo Jumapili iliyopita.

Wakimbizi wa Sudan Kusini nchini Uganda

Inakadiriwa kuwa, kila siku wakimbizi karibu elfu mbili wa Sudan Kusini huvuka mpaka na kuingia katika kambi ya wakimbizi ya Bidi Bidi nchini Uganda. Kwa sasa kambi hiyo ina wakimbizi laki mbili na asilimia 75 ya wakimbizi hao ni wanawake na raia wenye umri wa chini ya miaka 18.

Hii ni katika hali ambayo, siku chache zilizopita, Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini alisema taifa hilo changa zaidi barani Afrika litafanya uchaguzi mwaka ujao 2018, ambapo mbali na kutangaza kuwa binafsi atawania urais, alimtaka hasimu wake wa kisiasa Riek Machar kurejea nchini kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi huo.