Morocco, mwenyeji wa mkutano wa Umoja wa Vyuo Vikuu vya Kiislamu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i25188-morocco_mwenyeji_wa_mkutano_wa_umoja_wa_vyuo_vikuu_vya_kiislamu
Mkutano wa saba mkuu wa Umoja wa Vyuo Vikuu vya Ulimwengu wa Kiislamu katika kulinda utambulisho wa Kiislamu wa "Quds Tukufu" umefanyika nchini Morocco.
(last modified 2025-12-01T10:34:25+00:00 )
Feb 15, 2017 15:58 UTC
  • Morocco, mwenyeji wa mkutano wa Umoja wa Vyuo Vikuu vya Kiislamu

Mkutano wa saba mkuu wa Umoja wa Vyuo Vikuu vya Ulimwengu wa Kiislamu katika kulinda utambulisho wa Kiislamu wa "Quds Tukufu" umefanyika nchini Morocco.

Shirika la habari la IQNA limeripoti habari hiyo na kusema kuwa, wakuu wa vyuo vikuu vya ulimwengu wa Kiislamu wameshiriki kwenye mkutano huo na kuunga mkono hatua za Chuo Kikuu cha Quds huko Palestina cha kushikamana na muqawama na kusimama kidete kukabiliana na jinai za utawala ghasibu wa Israel na kulinda utambulisho wa Kipalestina na Kiislamu wa mji mtakatifu wa Baytul Muqaddas.

Washiriki wa mkutano huo wamehimiza mshikamano na kuwa kitu kimoja vyuo vikuu vya umoja huo na kukiunga mkono na kukisaidia kwa kila namna Chuo Kikuu cha Quds.

Baadhi ya washiriki wa mkutano wa ISESCO

 

Mkutano huo umezitaka pia taasisi za Kiarabu, Kiislamu na za kimataifa zinazohusiana na masuala ya elimu ya juu kuzisaidia taasisi za vyuo vikuu vya mji wa Baytul Muqaddas na Palestina kiujumla, hususan Chuo Kikuu cha Quds.

Mkutano Mkuu wa Umoja wa Vyuo Vikuu vya Ulimwengu wa Kiislamu umefanyika tarehe 13 na 14 mwezi huu wa Februari nchini Morocco, kwa kuwashirikisha wakuu vya vyuo vikuu mbalimbali vya ulimwngu wa Kiislamu akiwemo Muhammad Kafi, mkuu wa Chuo Kikuu cha Firdousi cha mjini Mash'had Iran.

Umoja wa Vyuo Vikuu vya Ulimwengu wa Kiislamu uliasisiwa mwaka 1987 chini ya Taasisi ya Kiislamu ya ISESCO na hivi sasa vyuo vikuu na taasisi 314 za elimu ya juu ni wanachama wa umoja huo.