Feb 17, 2017 14:35 UTC
  • Waziri ajiuzulu Sudan Kusini, ajiunga na kundi la waasi

Waziri wa Leba wa Sudan Kusini ametangaza kujiuzulu na kusema kuwa sasa ataunga mkono harakati zinazofanywa na waasi wanaomuunga mkono Riek Machar, Makamu wa Rais wa zamani wa nchi hiyo.

Katika barua yake ya wazi ya kujiuzulu, Luteni Jenerali Gabriel Duop Nam, amesema kuwa: "Nimejivua wadhifa wa Waziri wa Leba, kuanzia sasa, nitaonyesha utiifu wangu na kufanya kazi bega kwa bega na Dakta Riek Machar."

Kamanda huyo wa zamani wa jeshi kadhalika amepongeza uongozi wa Machar na kusisitiza kuwa atashirikiana naye kikamilifu katika kila hatua ya kuikomboa tena nchi hiyo.

Waziri huyo wa Leba wa Sudan Kusini, Luteni Jenerali Gabriel Duop Nam amejiuzulu chini ya wiki moja, baada ya Luteni Jenerali Cirillo Swaka, kamanda mwingine wa ngazi za juu kutangaza kujiuzulu wadhifa wake wa Mkuu wa Idara ya Lojistiki ya Jeshi la nchi hiyo.

Rais Salva Kiir na aliyekuwa makamu wake Riek Machar

Haya yanajiri siku chache baada ya António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kueleza wasi wasi kuhusu hali ya mambo katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika akionya kuwa, kushadidi mapigano katika maeneo mawili ya Wau Shilluk kwenye mkoa wa Upper Nile na Kajo Keji katika eneo la Equatoria ya Kati kutakuwa na maafa makubwa kwa raia wa maeneo hayo.

Licha ya hali hii, Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini amesisitiza kuwa atawania kiti cha rais kwa muhula mwingine katika uchaguzi mkuu unaotazamiwa kufanyika mwaka ujao 2018; huku akimtaka aliyekuwa makamu wake, Riek Machar akomeshe uasi na kurejea nchini kushiriki uchaguzi huo.

Tags