Sababu ya kuendelea hujuma za kigaidi Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i25436-sababu_ya_kuendelea_hujuma_za_kigaidi_somalia
Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa Somalia Michael Keating amelaani hujuma ya kigaidi iliyojiri Jumapili katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu huku wengi wakihoji sababu ya kuendelea hujuma za kigaidi nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 21, 2017 04:21 UTC
  • Sababu ya kuendelea hujuma za kigaidi Somalia

Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa Somalia Michael Keating amelaani hujuma ya kigaidi iliyojiri Jumapili katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu huku wengi wakihoji sababu ya kuendelea hujuma za kigaidi nchini humo.

Keating amesema kuuawa raia ni jambo la kuchukiza na linaloonyesha kuwa magaidi na wale wenye misimamo mikali hawajali maisha wala masaibu ya raia wa kawaida.

Watu wasiopungua 39  wanasadikiwa kuuawa  wakati gari lililokuwa limesheheni mabomu liliporipuka katika makutano ya barabara ya mtaa wa Madina mjini Mogadishu. Mlipuko huo ulikuwa hujuma ya kwanza kubwa kujiri Somalia tokea aingie madarakani rais mpya wa Somalia Mohammad Abdullahi Mohamad, maarufu kama Farmaajo, mnamo Februari 8. Magaidi wakufurishaji wa kundi la Al Shabab hutekeleza mashambulizi ya mara kwa mara mjini Mogadishu, mji ambao unalindwa na askari wa Umoja wa Afrika maarufu kama AMISOM. Magaidi wa Al Shabab wamepoteza baadhi ya maeneo waliyokuwa wakiyadhibiti kusini mwa Somalia hasa mji mkuu Mogadishu lakini wangali wanashikilia maeneo makubwa ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika. Lakini pamoja na kupoteza maeneo waliyokuwa wakiyashikilia, magaidi wa Al Shabab bado wanamiliki silaha na zana za kivita ambazo wanatumia kushambulia maeneo ya Somalia na hata nchi jirani ya Kenya.

Baadhi ya weledi wa mambo wanasema baada ya kupoteza  maeneo waliyokuwa wameyateka, magaidi wa Al Shabab sasa wanatekeleza mashambulizi ya kuvizia huku na kule na wanafanikiwa katika ugaidi wao huo kwa sababu wanachanganyika na raia wa kawaida na hivyo kuwa vigumu kuwatambua. Magaidi wa al Shabab pia wamezidisha hujuma zao dhidi ya raia na askari wa kigeni nchini Somalia hasa dhidi ya askari wa Kenya ili kuiweka serikali ya Nairobi chini ya mashinikizo na hatimaye ilazimike kuondoa askari wake katika kikosi cha AMISOM. Itakumbukwa kuwa hivi karibuni makumi ya askari wa Kenya waliuawa katika hujuma ya Al Shabab katika eneo la Kulbiyow, Somalia ikiwa ni mwaka mmoja baada ya askari wengine zaidi ya 100 kuuawa katika hujuma ya kundi hilo la kigaidi katika eneo la El Adde huko huko Somalia.

Lakini swali ambalo weledi wengi wa mambo ya kisiasa wanauliza ni hili kuwa je, ni kwa nini pamoja na kuwepo muungano wa kimataifa dhidi ya Al Shabab bado kundi hilo halijashindwa? Je, kundi hilo la magaidi wakufurishaji linapata silaha na kuimarishwa na nani hasa:

Inaelekea kuwa madola makubwa yaliyo nje ya eneo, yaani madola ya nchi za Magharibi ndio wahusika wakuu katika mgogoro wa Somalia. Nchi za Magharibi zinafuata sera za undumakuwili kuhusu Somalia. Ni wazi kuwa Somalia ina umuhimu mkubwa kwa nchi za Magharibi kwa sababu kadhaa na kwa msingi huo madola hayo ya kibeberu yanataka kueneza ushawishi na satwa yao nchini humo na eneo zima la Pembe ya Afrika. Kwa msingi huo nchi za Magharibi zinataka kundi la Al Shabab liendeleze ugaidi wake Somalia ili madola hayo ya kibeberu yapate kisingizio cha kutuma majeshi yao katika nchi hiyo au kuweka vituo vya kijeshi katika eneo hilo la kistratijia. Somalia ni nchi yenye utajiri wa mafuta na gesi mbali na kuwa katika eneo la kistraijia la Lango Bahari la Babul Mandab ambalo ni muhimu kwa meli za mafua na kibiashara zinazotoka Ghuba ya Uajemi kuelekea Bahari ya Sham na hatimaye katika Bahari ya Mediterenea na Bara  Ulaya.

Rais mpya wa Somalia Mohammad Abdullahi Mohamad, maarufu kama Farmaajo

Kwa maelezo hayo inatubainikia wazi sababu ya nchi za Magharibi kuitazama Somalia kama nchi inayopaswa kuwa chini ya udhibiti na satwa yao. Nchi za Magharibi hivi sasa zinajenga kituo cha siri cha kijeshi katika eneo lenye mamlaka ya ndani la Somaliland kwa lengo la kuimarisha udhibiti wao wa Lango Bahari la Babul Mandab ambalo kwa hakika ni mshipa muhimu wa uchumi wa dunia.