Wanajeshi wa Niger washambuliwa katika mpaka wa Mali
Wanajeshi kadhaa ya Niger wameuawa na wengine kujeruhiwa katika shambulio la kigaidi karibu na mpaka wa nchi hiyo na Mali.
Toure Seydou Albdoula Aziz, msemaji wa jeshi la Niger ametangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, wanajeshi 15 wa nchi hiyo waliuawa na 19 wengine kujeruhiwa wakati watu wenye silaha waliposhambulia doria ya askari hao.
Maeneo ya magharibi mwa Niger kwa miaka mingi sasa yanashuhudia mashambulizi ya mara kwa mara ya makundi yenye misimamo mikali na wengi wa washambuliaji huwa wanatokea kaskazini mwa nchi jirani ya Mali.
Mwezi Machi 2012 maeneo ya kaskazini mwa Mali yalitekwa na makundi yenye misimamo mikali lakini mwezi Januari 2013 wanajeshi wa kimataifa waliwafurusha magaidi hao kutoka katika baadhi ya maeneo waliyoyateka. Hadi leo hii kuna maeneo kadhaa ya kaskazini mwa Mali bado yako mikononi mwa waasi.
Niger inashuhudia pia mashambulizi ya mara kwa mara ya genge la kigaidi la Boko Haram. Genge hilo lilianzisha machafuko katika nchi jirani ya Nigeria mwaka 2009 na hadi hivi sasa raia wengi wameshauawa na maelfu ya wengine kupoteza makazi yao.