UN yataka Morocco, Polisario kupunguza uhasama
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameelezea wasiwasi wake kuhusu kuendelea kwa mvutano kwenye ukanda unaotenganisha pande hasimu huko Sahara Magharibi.
Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imemnukuu Bwana Guterres akieleza kuwa mvutano huo ni kati ya vikosi vya Morocco na vile vya Harakati ya Polisario ambavyo vimekaribiana tangu mwezi Agosti mwaka jana na kuleta wasiwasi mkubwa.
Pande mbili hizo zimekuwa zikifuatiliwa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa huko Sahara Magharibi, MINURSO.
Katibu Mkuu ametoa wito kwa pande hizo kujizuia kuchukua hatua yoyote iwe ya kijeshi au kupitia raia, hatua ambazo amesema zinaweza kuongeza mvutano.
Amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha magari binafsi yanayopita eneo hilo hayazuiwi na kwamba isichukuliwe hatua yoyote ya kubadili hali iliyokubaliwa kuwepo kwenye ukanda huo usio na mapigano.
Badala yake ametaka pande hizo kuondoa vikosi vyao haraka iwezekanavyo na kuweka mazingira bora ya kurejesha mazungumzo kwa minajili ya mchakato wa kisiasa, mpango unaoongozwa na Umoja wa Mataifa.
Hayo yanajiri wakati ambao Mfalme wa Morocco ameuandikia barua Umoja wa Mataifa akiishtaki Harakati ya Polisario kwa kile alichokiita kuwa hatua za kichochezi za harakati hiyo.
Mwaka 1984 Morocco ilijiondoa katika Umoja wa Afrika AU, wakati huo ukijulikana kama OAU, baada ya eneo la Sahara Magharibi, lililojitenga na Morocco, kukubaliwa kama mwanachama wa umoja huo. Morocco ilichukua udhibiti wa Sahara Magharibi kutoka mikononi mwa mkoloni Mhispania mwaka 1975 na inasisitiza kuwa eneo hilo ni sehemu ya ardhi yake.
Mwezi uliopita Umoja wa Afrika AU ulikubali tena uanachama wa Morocco baada ya miaka 33 wakati nchi hiyo ilijiondoa katika umoja huo kutokana na mgogoro wa Sahara Magharibi ambao hadi sasa haujatatuliwa.